Mvua kubwa yamiminika Somalia

Watu waliokimbia ukame nchini Somalia katika makambi karibu na Mogadishu wamekumbwa na mvua kubwa kwa siku kadhaa sasa.

Wafanyakazi wa kutoa misaada wamesema watu watano, wakiwemo watoto watatu, wamefariki dunia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Somalia

Daktari ameiambia BBC watu walishindwa kupata hifadhi kutokana na mvua na baridi.

Waathirika hao wamelazimika kuhama makazi yao kutokana na ukame uliokumba maeneo mengi ya pembe mwa Afrika.

Takriban watu milioni 10 wameathiriwa katika eneo hilo.

Osman Duflay, daktari wa Mogadishu, alisema wakaazi walioko makambini wanakabiliwa na "maafa".

Alisema, " Hasa watoto wenye chini ya umri wa miaka mitano na mama wajawazito, wana utapiamlo na maradhi ya kuambukiza kama vile surua, kuhara na kifua."

Mapema wiki hii Mark Bowden, msimamizi wa masuala ya kibinadamu wa umoja wa mataifa wa Somalia, aliiambia BBC nchi hiyo inakaribia kuwa na baa la njaa.

Alisema, "Miezi michache ijayo ni muhimu sana."

Wiki iliyopita wapiganaji wa kundi la Kisomali la al-Shabab- wanaopigana na serikali ya Mogadishu- lilisema litaanza kuruhusu mashirika ya kigeni ya kutoa misaada ilimradi tu hawatoonyesha kuwa na "ajenda ya siri."