Waziri Mkuu wa Uingereza barani Afrika

Waziri Mkuu wa Uingereza Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri Mkuu wa Uingereza

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuingilia kijeshi mzozo wa Libya sio utaratibu ufaao wa kutatua mzozo wa nchi hiyo.

Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari mjini Pretoria akiandamana na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, Bw. Zuma amesema hatma ya Kanali Gaddafi inafaa kuamuliwa kwa kufanya majadiliano.

Waziri Mkuu Cameron amesema kuwa kuna tofauti kati ya viongozi wa Afrika na shirika la kujihami la Nato juu ya operesheni za kijeshi zinazoendelea nchini Libya.

Cameron yuko Johannesburg katika mwanzo wa ziara yake ya kuimarisha ushusiano wa kibiashara kati ya Uingereza na Afrika.

Waziri mkuu Cameron amesema kuwa NATO na viongozi wa Afrika wote wana lengo moja ambalo ni kumtaka kanali Gaddafi ang'atuke mamlakani.

Lakini Rais Zuma amesema mashambulio ya bomu ya NATO hayajasaidia hali ya siasa nchini Libya na amekariri wito wa Muungano wa Afrika wa mazungumzo kuhusu kuondoka kwa Kanali Gaddafi.

Na wakati huohuo ziara ya Cameron imekatizwa ili arejee nyumbani kukabiliana na mzozo unaoendelea kutokota wa udukuzi na waandishi wa habari.

Mwandishi wa BBC wa masuala ya siasa James Landale amesema ziara hii hapo awali ilipangiwa kuwa ya siku tano badala ya siku mbili jambo litakalomfanya atembelee nchi mbili tu ikiwa ni Afrika Kusini na Nigeria.

Bw Cameron anakabiliwa na wakati mgumu kuhusu uwamuzi wake wa kumuajiri aliyekuwa mhariri wa News of the World Andy Coulson kuwa msemaji wake. Bw Coulson ambaye hatumiki tena Kama msemaji wa Waziri Mkuu alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana katika uchunguzi unaoenedelea kwa waandishi wa gazeti hilo kutokana na udukuzi wao waliofanya katika simu za watu. Katika ziara hii, Bw Cameron anatarajiwa kuunga mkono mpango wa biashara huru kwa mataifa 26 ya Afrika utakaojumuisha eneo linalokaliwa na zaidi ya watu milioni 600 ikiwa ni zaidi ya nusu ya eneo la bara la Afrika katika kipindi cha miaka mitatu.

Amesema mpango huo utaongeza pato la bara hilo na kufika dola bilioni 62 ikiwa ni dola bilioni 20 zaidi ya bajeti ya kila mwaka ya msaada kwa eneo a Afrika lililo kusini mwa jangwa na Sahara.

Ziara ya wiki hii ni moja wapo ya ziara za hivi karibuni za kibiashara ambapo Waziri Mkuu Cameron amekwenda China na India na naibu wake Nick Clegg ametembelea nchi za Mexico na Brazil.Hizi ni hatua za kuleta uhusiano wa karibu na mataifa yanayokua kiuchumi ambayo yanaonesha kuongoza katika nyanja hiyo katika miaka ijayo.