Hofu yazuka kuhusu afya ya Hosni Mubarak

Kumekuwa na habari za kutofautiana kuhusu hali ya afya ya aliyekuwa rais wa Misri Hosni Mubarak, baada ya wakili wake kudai kuwa alizirai na kupoteza fahamu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Madaktari wa Mubarak wanakanusha kuwa amepoteza fahamu

Kituo cha kitaifa cha televisheni nchini Misri ndicho kilikuwa cha kwanza kutangaza taarifa hiyo ya wakili wake.

Hata hivyo taarifa hiyo imekanushwa na madaktari kadhaa ambao wamekuwa wakimhudumia Bw Mubarak.

Daktari anayeongoza jopo hilo linalo mhudumia amesema kuwa hali yake ni nzuri na kuwa haijazorota kama ilivyodaiwa.

Dakatari huyo ameelezea kuwa Hosni Mubarak, alikuwa anasikia kizunguzungu baada ya kasi ya msukumo wa damu kupungua lakini sasa amepata tiba ya tatizo hilo.

Rais huyo wa zamani amelazwa kwenye hospitali moja huko Sham el Sheikh na anatarajiwa kufika mahakamani mwezi ujao kujibu mashataka ya ufisadi na kuamrisha waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wake wauawe.

Wafuasi wa upizani wanaamini kuwa viongozi wa kijeshi hawataki kesi hiyo dhidi ya Mubarak iendelee kwa kuwa huenda yatakayo fichuliwa yatawaaibisha.

Taarifa hizi sasa huenda zikachochea zaidi hofu watu walionayo kuhusu afya ya Hosni Mubarak ambaye ameugua kwa muda mrefu sasa.