Barcelona kutokata tamaa kwa Fabregas

Kocha wa Barcelona Pep Guardiola amesema klabu yake "itapigana hadi mwisho" mpaka imnase kiungo wa Cesc Fabregas.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Cecs Fabregas

Mabingwa hao wa Ulaya mwezi wa Juni mwaka huu waliweka dau la paundi milioni 27 kwa ajili ya kumsajili Fabregas, lakini dau hilo lilikataliwa na Arsenal.

"Barcelona imetoa maombi mengine kwa Arsenal na tuna muda hadi tarehe 31 mwezi wa Agosti kujaribu kufikia makubaliano," alisema kocha huyo wa Barca Guardiola.

"Tunaendelea kupigana hadi mwisho kujaribu kumpata Cesc kwa sababu tunaamini ataisaidia timu na kikosi kizima."

Ameongeza: "Kuna kiasi cha pesa kwenye hazina yetu zinasubiri kumsajili Fabregas, lakini iwapo haitawezekana pesa hiyo itatumika kwa nyingine."

Fabregas ni zao la chuo cha vijana wa Barcelona kabla ya kujiunga na Arsenal akiwa na umri wa miaka 16 mwaka 2003. Hakusafiri na kikosi cha Arsenal kilichokuwa bara Asia kwa mazoezi ya kujinoa kwa ligi.

Mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Barcelona Andoni Zubizarreta, amesema jukumu kubwa la timu hiyo kabla ya kukamilika usajili ni kumpata mshambuliaji mpya, huku wakimlenga zaidi mshambuliaji wa Udinese anayechezea pia timu ya taifa ya Chile Alexis Sanchez.