Wajumbe wa marekani na libya wakutana

Maafisa wa Libya na Marekani wamefanya mazungumzo huku majeshi ya NATO yakiendelea kuishambulia nchi hiyo ili kuiangusha serikali ya Kanali Gaddafi.

Image caption waasi wanadai kuwashinda nguvu wanajeshi wa serikali mjini Brega

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kufanyika kwa mkutano huo wa siku moja wiki iliyopita.

Lakini Marekani imesisitiza kuwa hakuna majadiliano mengine isipokuwa kung'oka madarakani kwa kiongozi huyo wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

Msemaji wa serikali ya Libya Moussa Ibrahim ameyasifu mazungumzo hayo akisema ni hatua muhimu katika kurekebisha uhusiano kati ya Libya na Marekani.

"Tunaunga mkono mazungumzo na juhudi zote za amani bora wasiamue hatma ya Libya kule nje," aliambia wandishi wa habari mjini Tripoli.

Wakati huo huo mapigano yameendelea katika mji wa Brega ambapo waasi wamekuwa wakipambana na kujaribu kuwaondoa majeshi ya Gaddafi tangu alhamisi.

waasi wanadai kuwa wamefaulu kuyasukuma majeshi ya serikali had maeneo ya Ras Lanuf baada ya kuteka tena sehemu kubwa ya mji wa Brega.

Lakini serikali imekanusha madai hayo ya waasi.

Utawala katika mji wa Brega ulioko kilometa 750 kutoka mji mkuu Tripoli umebadilika mara kadhaa tangu mapambano kati ya serikali ya waasi yaanze mwezi Februari.

Wadadisi wanasema waasi wakifaulu kuuteka mji huo hatua hiyo itakua pigo kubwa sana kwa serikali ya Kanali Muammar Gaddafi.

Rais Jacob Zuma wa Afrika kusini ametofautiana wazi na waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kuhusu hatma ya Libya.

Rais Zuma amesisitiza kuwa Libya inahitaji utawala wa kidemokrasia lakini lazima suluhu itoke kwa raia wenyewe na sio shinikizo kutoka nchi za ng'ambo au kupitia mashambulio yanayoendelezwa na wanajeshi wa NATO.