Leeds United kuanza msimu na majeruhi

Leeds United huenda ikauanza msimu wa Ligi bila ya washambuliaji wake wawili muhimu Luciano Becchio na Davide Somma kuumia.

Image caption Wachezaji wa Leeds United

Becchio mshambuliaji kutoka Argentina anahitaji kufanyiwa upasuaji wa goti wakati Somma kutoka Afrika Kusini hatacheza soka kati ya miezi sita hadi tisa kutokana na kuumia goti.

Meneja wa Leeds United Simon Grayson ameeleza katika mtandao wa klabu: "Kwa sasa tunapima hali itakavyokuwa kwa Becchio iwapo anahitaji upasuaji au la."

"Tutajua zaidi katika siku chache zijazo hali itakavyokuwa."

Becchio, mwenye umri wa miaka 27, msimu uliopita alifunga mabao 20 lakini hakuweza kucheza katika michezo ya mwisho kumalizia msimu kutokana na matatizo ya msuli wa paja.

Grayson pia anakabiliwa na hatari ya kumkosa Somma kwa karibu msimu mzima, baada ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Afrika Kusini kuumia goti wakati wa mazoezi ya kujinoa kwa msimu huu.

Kocha huyo wa Leeds wiki hii amewapiga marufuku wachezaji wake kutumia mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya Somma kubainisha kuhusu kuumia kwake.