Wachezaji wa Zambia na kifungo cha nje

Wachezaji saba wa Zambia waliojihusisha na kashfa ya kupanga matokeo nchini Finland wamehukumiwa kifungo cha nje.

Image caption Wachezaji wa Zambia

Mahakama imewahukumu wachezaji hao saba wa Zambia kifungo cha nje cha kati ya miezi sita hadi 20 kutokana na kujihusisha na kashfa hiyo.

Raia wa Singapore ambaye alikuwa kiini cha kashfa hiyo, Wilson Raj Perumal, amehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela.

Mahakama imesema Perumal alijipatia dola 210,000 kwa kupanga matokeo ya mechi za ligi ya Finland tangu mwaka 2008.

Wachezaji hao wa Zambia ni Godfrey Chibanga, Chileshe Chibwe, Francis Kombe, Stephen Kunda, Christopher Musonda, Chanda Mwaba na Nchimunya Mweetwa, wanaochezea timu ya Rovaniemi Palloseura (RoPs), walihukumiwa pamoja na wachezaji wenzao wawili wa Georgia.

Wachezaji hao sasa wapo huru kuondoka Finland lakini mustakabali wao kisoka haujulikani kutokana na kuwepo uwezekano wa kukabiliwa na adhabu kutoka Fifa.

Wametuhumiwa kukubali kupokea rushwa ya kati ya dola 15,000 hadi dola 57,000 kila mmoja ili kupanga matokeo ya michezo.

Perumal ametiwa hatiani kwa rushwa, kughushi na kuingia nchini humo kinyume na sheria.

Raia huyo wa Singapore pia anatuhumiwa na Shirikisho la Soka duniani Fifa kwa kupanga mechi za taifa za Afrika na Asia.

Perumal alikamatwa Finland mwezi wa Februari baada ya kuingia nchini humo akiwa na hati ya kusafiria ya kughushi.

Alituhumiwa kuwa kinara wa kupanga mechi kwa timu ya kaskazini mwa Finland katika mji wa Rovaniemi.

Mahakama hiyo imesema mechi 24 za Rovaniemi zilipangwa matokeo yake na Perumal ilithibitishwa kujihusishwa kupanga matokeo ya mechi saba.

Pia alipanga mechi mbili za ligi ya Finland, ikihusisha timu za Oulu na Mariehamn.

Ligi ya Finland imegubikwa sana na kashfa ya upangaji wa matokeo tangu ilipoanza mwezi wa Mei.