Mabaki ya msaidizi wa Hitler yafukuliwa

Kaburi ambalo limekuwa na mabaki ya msaidizi wa Adolf Hitler, Rudolf Hess, limebomolewa, ili kuyazuia makundi ya ki-Nazi ambayo yamekuwa yakilitembelea na kutoa heshima zao kuacha kufanya hivyo.

Mifupa ya Hess ilifukuliwa kutoka kaburi moja mjini Wunsiedel, eneo la Ujerumani kusini, mapema siku ya Jumatano.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Makundi yanayounga mkono ubaguzi wa rangi yamekuwa yakilitembelea kaburi hilo

Mifupa hiyo itateketezwa, na jivu kutawanywa baharini.

Hess alikamatwa baada ya kuingia kwa ndege nchini Uingereza mwaka 1941, na kuhukumiwa kifo.

Alijinyonga gerezani mjini Berlin, Ujerumani, mwaka 1987, akiwa na umri wa miaka 93.

Kabla ya kifo chake, aliandika wasia azikwe katika mji mdogo wa Wunsiedel, ambako familia yake ilikuwa na nyumba walioitumia kwa mapumziko, na wazazi wake walikuwa tayari wamezikwa hapo.

Kanisa la Lutherani wakati huo lilikubali ombi lake, likiamua kwamba haliwezi kupuuza mapendekezo ya marehemu.

Lakini kanisa hilo na wakaazi wa hapo wamekuwa wakiishi kwa hali ya wasiwasi, kufuatia makundi mbalimbali ya ubaguzi wa rangi kulitembelea kaburi hilo mara kwa mara.

Kila mwaka, katika kumbukumbu za kifo chake, makundi yanayosifu shughuli za ki-Nazi yamekuwa yakifika hapo kutoa heshima zao, na vile vile kuweka maua hapo.