Marekani kusaidia baa la njaa Somalia

Image caption Marekani kupeleka msaada wa chakula maeneo ya al-Shabaab

Marekani imesema itatuma msaada katika eneo lililokumbwa na baa la njaa nchini Somalia linalodhibitiwa na kundi la kiislam la al-Shabaab

Lakini Maafisa wa misaada wa Marekani wamesema ni lazima wapewe uhakika kuwa wapiganaji hao hawataingilia kati kuvuruga ugawaji wa misaada hiyo.

Marekani inalichukulia kundi la al-Shabab kuwa la kigaidi na mwaka jana kundi hilo lilizua msaada wa chakula katika eneo kubwa la Somalia linalolidhibiti.

Umoja wa Mataifa umetangaza rasmi kuwa kuna baa la njaa katika maeneo mawili ya Kusini mwa Somalia yaliyokumbwa na ukame mkali kwa zaidi ya karne.

Al-Shabab, kundi linalojihusisha na al-Qaeda linadhibiti sehemu kubwa ya Kusini na Katikati mwa Somalia, limezuia huduma ya mashirika ya misaada katika eneo lake tangu mwaka 2009, lakini hivi karibuni liliruhusu misaada hiyo ianze kutolewa.

Naibu Kamishna wa Shirika la Maendeleo la Marekani, Donald Steinberg, amesema misaada hiyo isiwanufaishe al-Shabab.

"Tunachokihitaji ni Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na mashirika mengine, Umoja wa Mataifa au mashirika mengine, yote ya umma na sekta binafsi ambao wako tayari kwenda Somalia watupatie uhakika kuwa hawajasumbuliwa na al-Shabab, na kwamba hawajapewa vishawishi vyovyote kutoka kwa al-Shabab, ili tuweze kufanya kazi bila kuingiliwa," Bw Steinberg ameiambia BBC.

Amesema lengo lilikuwa ni kuokoa maisha, "na sio kucheza mchezo wa ‘paka na panya’ na mashirika ya UN au kundi lolote lingine ambalo lina ujasiri wa kutosha kwenda na kutoa msaada huo.

Mchambuzi wa BBC Afrika Martin Plaut anasema hatua hii inaonyesha mabadiliko makubwa katika sera za Washington.

Mwezi April 2010 Rais wa Marekani Barack Obama alitoa maagizo maalum yakilitaja kundi la al-Shabab kuwa ni kundi la kigaidi, akimaanisha hakuna msaada wowote utakaopelekwa katika eneo linalodhibitiwa na kundi la al-Shabaab, anaongeza mchambuzi wa BBC.

Inakadiriwa kuwa watu milioni 10 wameathiriwa na ukame mbaya eneo la Pembe ya Afrika kwa muda wa zaidi ya karne. Zaidi ya raia wa Somalia 166,000 inaripotiwa kuwa wameyakimbia makazi yao na kuingia nchi za Kenya na Somalia.