Waliokufa Malawi wazikwa leo

Mandamano Malawi Haki miliki ya picha AP
Image caption Mandamano Malawi

Maafisa wa utawala katika mji wa kaskazini wa Mzuzu wamesema kuwa Rais Mutharika amewazuia kufanya mazishi ya wengi ili kuepusha ghasia zaidi katika eneo hilo.

Waombolezaji walikusanyika asubuhi wakitaka kufanya mazishi ya pamoja kwa waliouawa katika mzozo huu wa sasa.

Na wakati huohuo jeshi limepelekwa katika miji mitatu ya Malawi kukabiliana na wanaoandamana kuipinga serikali ambapo watu 18 wameuawa. Rais Bingu wa Mutharika ameapa kutumia mbinu zote kukomesha maandamano hayo.

Waandamanaji wanamshutumu kwa kuitumbukiza Malawi katika mzozo huu wa kiuchumi unaoikumba nchi hiyo, ikiwa ndio mbaya zaidi kuwahi kutokea tangu nchi hiyo ijinyakulie uhuru wake.

Jeshi limepekwa katika mji mkuu wa Lilongwe, Blantyre na mji wa kaskazini wa Mzuzu. Wanajeshi wanakisaidia kikosi cha polisi wa kuzima ghasia katika miji hiyo mitatu.

Wizara ya afya imesema kuwa watu 18 wameuawa katika siku mbili za maandamano. Watu tisa waliuawa katika mji wa Mzuzu, sita Lilongwe na wawili Blantrye na mmoja katika mji wa Karonga unaopakana na Tanzania, idadi hii imetolewa na msemaji wa Wizara ya Afya Henry Chimbali. Wengine 44 walipata majeraha ya risasi katika mapambano kati ya waandamanaji na vikosi vya Polisi.

Msemaji wa Polisi amesema kuwa vikosi vya Polisi vilifyatua risasi mjini Lilongwe kuepusha wezi kuvamia maduka na magari.

Makundi ya kutetea haki za binadamu yalioandaa maandamano hayo ya kitaifa yamesema kuwa Malawi inakabiliwa na msururu wa majanga.

Gharama ya maisha imepanda na nchi hiyo inakabiliwa na upungufu wa mafuta, umeme na fedha za kigeni. Makundi hayo yameishutumu serikali kwa kukosa kusikia vilio vya watu na yanahofia Malawi huenda ikageuka kuwa taifa linalotawaliwa kimabavu.

Bw Mutharika - ambaye alichaguliwa mwaka 2004 - amesema anajiandaa kufanya mazungumzo na upinzani lakini nao unapaswa kukoma kuwatuma vijana barabarani kusababisha vurugu.