Huwezi kusikiliza tena

Kisa na Mkasa na Salim Kikeke

Kumpata mke balaa

Bwana mmoja nchini Marekani hatimaye amefunga ndoa kwa mara ya kwanza, baada ya kusaka mchumba kwa zaidi ya miaka sabini.

Bwana huyo Gilbert Harrick mwenye umri wa miaka tisini na tisa sasa ambaye alipigana katika vita vya pili vya dunia amesema hakuwahi kukutana na msichana aliyempenda kwa miaka yote hiyo.

Bwana Gilbert amefunga ndoa na Bi Virginia Hartman mwenye umri wa miaka themanini na sita.

Gazeti la Rochester Cronicle limesema wawili hao kwa sasa wanaishi katika nyumba ya kutunza wazee, mjini New York.

"Tulitaka tuishi pamoja katika chumba kimoja, lakini walitukatalia hadi tufunge ndoa" amesema bwana Gilbert, "Kwa hiyo nikamuomba tuoane na yeye akakubali" ameongeza mzee huyo.

Kabla ya kuoana na kuishi katika chumba kimoja, wapenzi hao walikuwa wakiandikiana barua za mapenzi kila mara.

"Ni wazimu, lakini ndio raha yenyewe" amesema Bi Virginia, ambaye ana watoto watano katika ndoa yake ya awali.

Chupi si lazima

Mamlaka za magereza katika jimbo la Florida zimeamua kubana matumizi kwa kuacha kutoa bure nguo za ndani kwa wafungwa.

Badala yake, mkuu wa gereza la Polk amesema kuanzia sasa wafungwa watalazimika kununua chupi ambazo awali zilikuwa zikitolewa bure.

"Hakuna sheria inayotulazimisha kuwapa wafungwa vazi hilo" amesema Liwali Grad Judd, ambaye pia ndio mkuu wa gereza hilo.

Gazeti la Telegraph limesema vivazi hivyo vya ndani vitawagharimu wafungwa hao dola mbili na nusu hadi dola nne na nusu kutegemea aina na mtindo.

Hata hivyo utawala wa gereza umesema si lazima wazinunue, wasiotaka kuvaa, wataachiwa wafanye hivyo.

Chupi hizi pia zitapatikana katika rangi moja tu, nyeupe.

"Wanaotaka watanunua, wasiotaka, basi waache upepo uingilie mguu mmoja na utokee mguu mwingine wa suruali" amesema Mkuu wa gereza.

Pombe ikizidi...

Haki miliki ya picha PA

Walevi wawili nchini Marekani waliingia matatani baada ya kuingia ndani ya karandinga la polisi ili wajipige picha kama vile wamekamatwa.

Wawili hao Ryan Letchford na Jeffrey Olsen waliingia katika gari la polisi lililokuwa limeegeshwa barabarani, na kuanza kupeana zamu kujipiga picha.

Hata hivyo shughuli hiyo iliingia doa wakati vitasa vya mlango wa gari vilipojifunga, wakati wawili hao wakiwa bado ndani ya karandinga.

Rafiki wa tatu wa jamaa hao alikuja kujaribu kuwatoa, lakini akashindwa na kulazimika kupiga simu polisi kuomba msaada.

Constable wa polisi Mike Connor ameliambia gazeti la kila siku la Philadelphia kuwa alifika na kuwafungulia walevi hao.

"Walikuwa wakiona aibu sana" amesema polisi huyo.

Hata hivyo wawili hao hawakuwa huru kwa muda mrefu, kwani walikamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya kutaka kuiba gari la polisi, ukorofi wa kihalifu na ulevi hadharani.

Makahaba kuchumbiwa

Kituo kimoja cha televisheni nchini zambia kimeanzisha kipindi kinachosaidia wasichana waliokuwa makahaba zamani, kutafuta wachumba.

Wasichana hao wapatao kumi na wanane mbali na kusaidiwa kutafutiwa wachumba, watapatiwa zawadi ya dola elfu tisa kila mmoja na pia kulipiwa gharama zote za harusi.

Kituo hicho kiitwacho Muvi TV, kimesema kinataka kuwapa wasichana hao nafasi ya kuanza maisha mapya.

Kipindi hicho kinaitwa "tayari kwa ndoa".

Mhubiri mmoja Mchungaji Jeff Musonda ametoa baraka zake kwa makahaba hao wa zamani.

Kituo hicho cha TV kimesema kiliwatafuta wasichana hao kutoka mitaa mbalimbali ya nchi hiyo.

Baadhi ya washiriki wamesema walikuwa wakiuza miili yao ili kuwahudumia watoto wao.

Hata hivyo watu wamepokea kwa hisia tofauti kipindi hicho, wengine wakisema mtu akishakuwa kahaba ni vigumu kubadilika kwa muda mfupi, huku wengine wakisema, hakuna haja ya kuwahukumu kwa mambo waliyoyafanya siku za nyuma.

Kulipa kulala jela

Haki miliki ya picha BBC World Service

Gereza moja nchini marekani mwishoni mwa wiki liliwatoza fedha watu kwa kulala ndani ya gereza.

Hiyo ilikuwa kwa watu waliokuwa wakitaka kuhisi maisha ya gerezani.

Gereza hilo Cole County, liliwatoza watu dola thelathini kwa usiku mmoja kwa watu waliotaka kuonja maisha ya jela siku ya Ijumaa na Jumamosi.

Maafisa wamesema nafasi hiyo imetolewa kwa wananchi ili kulijaribu gereza hilo jipya kabla halijaanza kazi rasmi ya kuwafungia wahalifu.

Shirika la habari la reuters limesema watu wapatao mia moja na sabini walifurika katika gereza hilo wakitaka kuona usingizi wa jela ukoje.

Baadhi ya watu waliofika kulala gerezani ni pamoja na mawakili na wanandoa waliokuwa wakiadhimisha miaka yao ya ndoa.

Watu hao walipitia misingi ya kuswekwa gerezani, ikiwa ni pamoja na kukaguliwa, kunyanganywa simu za mkononi, mikanda pamoja na vito walivyokuwa wamevaa.

Pia walipigwa picha kama wafungwa."Ingawa hakikuwa kifongo cha ukweli, lakini nilihisi kukosa uhuru" amesema Bob watson, mmoja wa watu waliolipa kulala jela.

Kila chumba kidogo ndani ya gereza hilo kina kitanda cha chuma na godoro jembamba, huku balbu yenye mwanga mdogo ikiwaka usiku kucha.

Hata hivyo kuna TV yenye channel moja ambayo haisikiki kutokana na kelele ndani ya gereza.

Na kwa Taarifa yako... Konokono anaweza kupita kwenye ncha ya wembe bila kujikata.

Tukutane wiki ijayo... Panapo majaaliwa....