Watu 308 wajeruhiwa mapambano Misri

Wizara ya Afya ya Misri inasema watu 308 walijeruhiwa katika mapambano Jumamosi, karibu na wizara ya ulinzi.

Haki miliki ya picha
Image caption Maandamano Misri

Wanajeshi walitumia magari na seng'enge, kuzinga mhadhara usifike makao makuu ya wizara mjini Cairo.

Watu wasiovaa sare ya polisi, tena waliwarushia mawe na mabomu waandamanaji.

Jeshi linasema washambuliaji walikuwa wenyeji, ambao hawakutaka mahema kupigwa kwenye mtaa wao, lakini waandamanaji wanasema, jeshi limeajiri wakora, kuwatisha.

Taarifa zaidi zinasema mamia ya waandamanaji wamerudi katika medani ya Tahrir, katikati mwaa mji wa Cairo, baada ya mapambano makali ya Jumamosi usiku.

Waziri wa Afya alisema, watu wengi walijeruhiwa wakati waandamanaji walipofanya mhadhara jana, hadi makao makuu ya halmashauri kuu ya jeshi inayotawala Misri.

Mohammed el-Baradei, aliyewahi kupewa tuzo nya Nobel ya amani, amesihi wakuu kutotumia nguvu dhidi ya maandamano ya amani.

Waandamanaji sasa wanaikaidi wazi halmashauri ya kijeshi inayotawala nchi, kwa mara ya kwanza tangu kuondoka kwa Rais Mubarak.

Kwa siku mbili mfululizo, walifanya mhadhara hadi makao makuu ya Wizara ya Ulinzi mjini Cairo.

Mbali ya vizuizi rasmi vilivowekwa na jeshi, waliwakuta wakora waliovaa kiraia, ambao waliwarushia mawe na mabomu ya moto, na waliwaandama watu kwa visu na fimbo.

Hizo ndio mbinu zilizotumiwa enzi za Hosni Mubarak, ingawa jeshi lili-wasifu wenyeji kwa kujitokeza kulinda mitaa yao.

Msemaji wa jeshi, alisisitiza kuwa jeshi lilikuwa vumilivu, lakini Mohammed el-Baradei, aliyepata tuzo ya amani ya Nobel, na anayetumai kugombea uongozi, ameisihi halmashauri ya jeshi, kuzuwia utumiaji wa nguvu dhidi ya maandamano ya amani.