Sudan yazindua sarafu mpya,baada ya Sudan Kusini

Nchi ya Sudan imezindua rasmi sarafu mpya.

Haki miliki ya picha wikipidia
Image caption Wasudan wakagua sarafu yao mpya

Kwa mujibu wa benki kuu nchini humo noti hizo mpya zinapatikana katika mabenki na sehemu za kubadilisha pesa.

Hatua hii ni jawabu kwa Sudan Kusini,ambayo ilijitenga wiki mbili zilizopita,na kuzindua sarafu yake.

Nchi zote mbili zitapata matatizo kiuchumi, kwa kuwa baadhi ya masuala ambayo hayajatatuliwa kati yao ni suala la matumizi ya fedha.

Benki kuu inatarajia kuwa noti zote za zamani zitaondolewa kwenye mzunguko katika muda wa miezi mitatu ijayo, lakini hio huenda ikawa ahadi ngumu kutimiza.

Wanasema sarafu hio mpya inaanzishwa kama 'hatua ya tahadhari', kwa kuwa Sudan Kusini tayari imetoa sarafu yake.

Inakisiwa kuwa kuna pauni za Sudan bilioni 2 kwenye mzunguko kwenye taifa hilo jipya, ambazo huenda zikaleta msukosuko kwa uchumi wa Sudan.

Huenda kukawa na mazungumzo zaidi na serikali ya Sudan Kusini juu ya noti za zamani nchini humo.

Haki miliki ya picha wikipidia
Image caption Wasudan Kusini Wafurahia sarafu yao

'Vita ya sarafu' " Tutachukua hatua zote za tahadhari ili kulinda uchumi wa Sudan,na tuna matumaini kuwa wote tutakubaliana juu ya mzunguko wa pauni Sudan Kusini," Naibu wa gavana Badr al-Din Mahmoud alisema katika taarifa.

Serikali ya Sudan inazungumza kwa tahadhari hawataki kusema kama kuna "vita ya sarafu" lakini hili ndilo hasa linalofanyika.

Wataalamu wa uchumi wanasema uchumi wa Sudan na pia Sudan Kusini utakuwa na matatizo kama hakuna ushirikiano kati yao.