Fifa yamtilia mashaka Abo Rida wa Misri

Hany Abo Rida raia wa Misri anakuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Fifa kuanza kutiliwa mashaka kutokana na tuhuma za rushwa.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Moja ya mikutano ya Fifa

Baada ya kumfungia maisha kujihusisha na soka Mohamed Bin Hammam siku ya Jumamosi, jaji kutoka Namibia anayeongoza Kamati ya Fifa ya Maadili, ametaka kufanyike uchunguzi zaidi.

Kamati ya jaji huyo Petrus Damaseb imeitaka idara ya sheria ya Shirikisho hilo la soka duniani, kuandaa mashauri dhidi ya maafisa walioambatana na Bin Hammam hadi Trinidad mwezi wa Mei.

Miongoni mwao ni Vernon Manilal Fernando wa Sri Lanka na Worawi Makudi kutoka Thailand.

Kama ilivyo kwa Abo Rida, wote wawili Fernando na Makudi ni wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa.

Viongozi kadha wa soka wa Caribbean pia wanatiliwa mashaka.

Siku ya Jumamosi, kamati ya Fifa ya maadili ilimtia hatiani Bin Hammam kwa kutoa rushwa wakati akiwania Urais wa Fifa kwenye uchaguzi mkuu wa Shirikisho hilo alipotembelea Port of Spain katika kisiwa cha Caribbean cha Trinidad.

Iwapo Fifa itafungua shauri dhidi ya Abo Rida, itakuwa na maana wajumbe wote wanne wa kamati ya utendaji ya Fifa kutoka Afrika watakuwa wameingia katika orodha ya kuchunguzwa tangu mwaka jana.

Mwaka jana mwezi wa Novemba Amos Adamu kutoka Nigeria alisimamishwa katika tume hiyo baada ya kupatikana na hatia ya kwenda kinyume na maadili ya Fifa.

Rais wa Shrikisho la Soka barani Afrika Issa Hayatou, kutoka Cameroon, na Jacques Anouma wa Ivory Coast wote walitiliwa mashaka mwezi wa Mei walipotuhumiwa kupokea pesa kutoka Qatar kwa ajili ya kuisaidi nchi hiyo ifanikiwe katika mbio za kuandaa Kombe la dunia mwaka 2022.

Tuhuma hizo, ambazo zimekanushwa vikali, ziliwekwa hadharani na Bunge la Uingereza baada ya gazeti la Sunday Times kuchapisha ushahidi kutokana na uchunguzi iliyofanya na kuupeleka Fifa.