Mputu kikosi cha DRC dhidi ya Senegal

Tresor Mputu Mabi amejumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kitakachopambana na Senegal kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza Kombe la Mataifa ya Afrika tarehe 3 mwezi wa Septemba.

Image caption Tresor Mputu Mabi

Mshambuliaji huyo wa klabu ya TP Mazembe Mputu Mabi kwa sasa anatumikia adhabu ya Fifa ya kusimamishwa kucheza soka, adhabu inayomalizika tarehe 11 mwezi wa Agosti.

Alifungiwa kucheza soka na Shirikisho hilo la soka duniani, baada ya kumshabulia kwa kumpiga mwamuzi wakati wa mashindano ya Kombe la Challenge kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati mwaka 2010.

Mchezaji mwenzake wa timu ya taifa Guy Lusadisu alifungiwa kwa miezi 11 kucheza soka.

Mputu Mabi ni miongoni mwa wachezaji 26 watakaounda kikosi cha timu ya taifa kilichotangazwa na kocha Robert Nouzaret.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa mchezaji bora wa soka barani Afrika mwaka 2009, amekuwa akifanya mazoezi na klabu yake wakati huu akiwa anatumikia adhabu yake.

Nouzaret amesisitiza kwamba kiwango cha Mputu Mabi kinampatia nafasi ya moja kwa moja kurejea katika timu ya taifa licha ya kutocheza mechi kwa mwaka mmoja.

Timu hiyo ya taifa ya Dr Congo itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Gambia tareh 10 mwezi wa Agosti siku moja kabla ya Mputu Mabi kumaliza adhabu yake.

Watasafiri kuelekea Senegal kuwakabili Simba hao wa Teranga wakiwa wanatafuta nafasi ya kucheza fainali za kuwania kombe la Afrika zitakazochezwa mwakani.