Libya yashtumu Uingereza kwa kutambua waasi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kanali Muammar Gaddafi

Serikali ya Libya imeshtumu uamuzi wa Uingereza kuwatambua waasi wa Libya kama "serikali yenye mamlaka" baada ya Ufaransa na Marekani kufanya hivyo pia.

Khaled Kaim, naibu waziri wa mashauri ya nchi za kigeni katika serikali ya Muammar Gaddafi,ameambia waandishi wa habari kwamba uamuzi huo si wa busara na ni wa kupotosha.

Libya itaomba mahakama ibatilishe uamuzi huo, alisema.

Uingereza imeamrisha kufukuzwa kwa wanadiplomasia wanane wa Gaddafi nchini humo.

Uongozi wa waasi, Baraza la utawala wa mpito (NTC), limempendekeza Mahmud Al-Naku, mwandishi wa habari, kama balozi mpya wa Libya mjini London.

Akizungumza na BBC alisema amekuwa uhamishoni kwa miaka 33 kwa sababu ya kupinga utawala wa Gaddafi.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa Uingereza William Hague amesema baraza hilo la mpito limeonyesha nia yake ya "kuwa na Libya yenye uwazi na demokrasia... tofauti na Gaddafi ambaye udhalimu wake dhidi ya watu wa Libya umemuondolea uhalali wa kutawala nchi".

Bendera ya kijani ya serikali ya Gaddafi bado ilikuwa inapepea nje ya ubalozi wa Libya eneo la Knightsbridge mchana wa Jumatano huku waandamanaji waliobeba bendera zenye rangi nyekundu, kijani na nyeusi za waasi wakikusanyika nje ya ubalozi huo.

Kufwatia uamuzi wa Marekani wa kutambua baraza la mpito wiki mbili zilizopita, BBC imefahamishwa kuwa Marekani imepata ''ombi rasmi'' kutoka kwa waasi kufungua tena ubalozi wa Libya mjini Washington.

Haki miliki ya picha AP
Image caption bendera ya waasi nchini Libya

Maafisa wa Marekani wanasema "wanatafakari" ombi hilo.

Waasi wa Libya na vikosi vinavyomuunga mkono Gaddafi bado wanapigana, miezi mitano tangu kuanza upinzani dhidi ya utawala wa miaka 42 wa Muammar Gaddafi, huku shirika la Nato likiendelea kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la kutoruhusu ndege kupaa juu ya anga ya Libya.