Kamanda wa waasi auawa Libya

Haki miliki ya picha wikipidia
Image caption Abdel Fattah Younes alimuasi Gaddafi na kujiunga na waasi

Kiongozi wa kijeshi wa waasi nchini Libya wanaokabiliana wakitaka kumpindua Kanali Muammar Gaddafi ameuawa, baraza la mpito la Libya limesema.

Kiongozi wa baraza hilo Mustafa Abdul-Jalil amesema Jenerali Abdel Fattah Younes ameuawa na watu wanaomuunga mkono Gaddafi, na kiongozi wa watu hao tayari amekamatwa.

Amesema Jenerali Younes aliitwa kwenye mkutano ambapo alitakiwa aeleze kuhusu harakati za kijeshi, lakini aliuawa kabla ya kufika kwenye kikao hicho.

Taarifa zinasema kuwa Jenerali Younes alishukiwa kuwa na uhusiano na majeshi yanayomuunga mkono Gaddafi.

Jenerali Younes ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani ambaye alikimbia na kujiunga na upande wa upinzani mwezi Februari.

Wasaidizi wawili wa Jenerali Younes, Kanali Muhammad Khamis na Nasir al-Madhkur, pia waliuawa kwenye shambulio hilo, Bwana Jalil alisema.

Taarifa ambazo hazikuweza kuthibitishwa zilisema kuwa Jenerali Younes na wasaidizi wake wawili walikamatwa mapema siku ya Alhamisi katika eneo la kaskazini mwa Libya.

Mapema siku ya Alhamisi, waasi walisema kuwa wameteka mji muhimu wa Ghazaya karibu na mpaka wa Tunisia, baada ya makabiliano makali na vikosi vya Kanali Gaddafi.