Malawi yaionya Nigeria isione ubwete

Rais wa Chama cha Soka cha Malawi, ameionya Nigeria kutoichukulia timu yake kama ni nyepesi watakapomenyana kuwania kufuzu kwa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2014.

Image caption Timu ya taifa ya soka ya Malawi

Timu ya taifa ya Nigeria maarufu Super Eagles kwa kiasi kikubwa inaonekana itashinda kundi la F ambalo pia zimo nchi za Ushelisheli ama Kenya na Djibouti au Namibia.

Lakini Walter Nyamilandu anahisi Malawi ina uzoefu na inaweza ikawaendesha mchakamchaka Wanigeria pamoja na umaarufu wao wa soka na pesa..

"Nigeria inaonekana kuwa na nafasi kubwa katika kundi hili lakini sisi ni timu ambayo hatuwezi kudharauliwa," alisema Nyamilandu.

Nyamilandu aliongeza kwamba Malawi mwaka mmoja uliopita ilitoa taarifa walipoweza kufanikiwa kucheza katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Angola.

"Kuna mapinduzi ya soka nchini Malawi; tupo katika nafasi nzuri sana sasa kuweza kufuzu kuelekea Gabon na Equatorial Guinea mwakani kwa ajili ya mashindano ya Mataifa ya Afrika."