Man United yailaza Barcelona 2-1

Bao la ushindi alilofunga Michael Owen dakika ya 76 liliiwezesha Manchester United kuwalaza mabingwa soka wa bara la Ulaya Barcelona 2-1 katika mchezo wa kirafiki wa kujiandaa kwa patashika za Ligi Kuu, uliofanyika mjini Washington DC.

Image caption Michael Owen baada ya kufunga bao la ushindi

Mbele ya mashabiki karibu 82,000, Nani alitangulia kuipatia Manchester United bao la kuongoza katika dakika ya 22.

Barcelona, ikicheza bila ya Lionel Messi, ilisawazisha katika dakika ya 70 kwa mkwaju wa Thiago Alcantara.

Owen alimiminiwa pande la Tom Cleverley na kupachika bao la ushindi wakati United wakikamilisha ziara ya Amerika Kaskazini na kushinda mechi zake zote tano ilizocheza.

Owen aliandika katika mtandao wa kijamii wa tweeter baada ya mchezo huo: "Kama ilivyo kawaida ya Barca, upande wa upinzani unapata shida sana kumiliki mpira! Na ndivyo ilivyokuwa katika mchezo wa leo! Nashukuru nimefanikiwa kufunga bao."

United walifungwa na Barcelona katika fainali ya Kombe la Ubingwa wa Ulaya katika uwanja wa Wembley mwezi wa Mei, ilionekana mabingwa hao wa soka wa England wakipata nafasi ndogo ya kulipiza kisasi.

Kikosi hicho cha Sir Alex Ferguson kitarejea nyumbani kujiandaa kwa mchezo wa kuwania Ngao ya Jumuia dhidi ya washindi wa Kombe la FA, Manchester City siku ya Jumapili ijayo katika uwanja wa Wembley.

Meneja msaidizi wa Manchester United Mike Phelan alisema: "Mechi ya usiku huu haikuwa ya kuwania kitu chochote. Ilikuwa muhimu kwamba wachezaji tuliowapanga walikuwa wanaelewa nini kinachohitajika unapopambana na timu bora duniani.

Pamoja na Messi kutocheza, Barcelona iliamua kutomchezesha Xavi, Carlos Puyol na Gerard Pique katika kikosi chao kilichoanza.