Mo Farah ajiandaa mbio za mita 10,000

Bingwa mara mbili wa Ulaya Mo Farah ameshinda mbio za mita 5,000m katika mashindano ya majaribio ya wanariadha wa Uingereza wanaojionoa kwa Ubingwa wa Dunia - baadae akatangaza atashiriki mbio za mita 10,000 tu zitakazofanyika Daegu, Korea Kusini.

Image caption Mo Farah

Farah alimaliza kwa kutumia dakika 14 sekunde 0.72 aliposhinda mbio za mita 5,000 ukiwa ushindi wake wa tisa mfululizo msimu huu.

"Nitajielekeza zaidi kwa mbio za aina moja na hizo ni mita 10,000," alisema Mo Farah mwenye umri wa miaka 28.

"Nitakwenda huko nikiwa na matumaini ya kushinda medali."

Farah amekuwa akifanya vizuri tangu alipohamia mji wa Portland, nchini Marekani pamoja na mkewe na mtoto wake, akifundishwa na mwalimu wake Alberto Salazar.

"Nimebadili mambo mengi katika maisha yangu, ukiwa mwanariadha unatakiwa wakati mwengine ujitoe muhanga," aliongeza.

"Mambo yanakwenda vizuri. Mashabiki wananiunga mkono sana, ambalo ni jambo zuri.

Wanariadha wawili walioshinda katika kila mchezo wakati wa mashindano hayo ya majaribio ya wanariadha wa Uingereza ndio watajihakikishia tikiti ya kwenda Daegu.