Brazil wana hamu kucheza na England

England huenda ikapambana na Brazil katika mchezo wa kirafiki wa ufunguzi wa mmoja wa viwanja vipya vitakaochezewa fainali za Kombe la dunia mwaka 2014.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Moja ya viwanja vya soka Brazil

Uwanja huo ambao unafanyiwa ukarabati mkubwa wa Mineirao katika mji wa Belo Horizonte utakamilika mwaka 2013 na katibu wa jimbo hilo anafikiri England ndio itakuwa timu muhimu ya kupambana nayo.

Sergio Barroso amesema: "Tunataka England kucheza na Brazil katika mchezo wa kirafiki kuufungua rasmi uwanja huo mpya."

Mechi ya mwisho kwa England katika mji wa Belo Horizonte ilikuwa mwaka 1950 walipofungwa 1-0 na Marekani katika Kombe la Dunia.

Uwanja huo unarekebishwa kuupa sura itakayovutia na kuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 65,000 na ndio utachezewa mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia mwaka 2014.

Lakini kuna wasiwasi kwamba Rais wa Chama cha Soka cha Brazil Ricardo Teixeira, huenda asiruhusu kufanyika mechi hiyo ya kujipasha moto, hasa ikizingatiwa maneno aliyotamka kuhusiana na England pamoja na vyombo vyake vya habari.

Teixeira, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Fifa, alisema Waingereza "walikuwa ni maharamia wanaotakiwa kwenda kuzimu".

Katibu Mkuu wa FA ya England, Alex Horne, wiki iliyopita alikwenda Rio de Janeiro kurekebisha uhusiano wa England na Brazil pamoja na Fifa, baada ya England kushindwa kupata nafasi ya kupata fursa ya kuandaa Kombe la Dunia la Mwaka 2018 .