Ukame Kenya Waturkana 14 wafa kwa njaa

Ukame umeathiri raia na wanyama nchini Kenya

Takriban watu 14 wamekufa katika eneo la Kaskazini Mashariki katika eneo la Turkana nchini Kenya, vifo vya kwanza kutokea vinavyohusiana na njaa nchini Kenya katika eneo linalohusiana na ukame.

Mbunge wa Turkana, John Munyes, alisema vifo hivyo vimetokea katika vijiji vitatu baada ya serikali kushindwa kusafirisha chakula kwa ajili ya watu walioathiriwa na ukame.

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya raia wa Kenya milioni nne wanatishiwa na ukosefu wa chakula katika eneo lilikumbwa na ukame mbaya katika kipindi cha miaka 60.

Nchi nyingine zilizoathiriwa ni Somalia, Ethiopia na Djiblouti.

Mwandishi wa BBC Odiambo Joseph akiwa Turkana anasema ametembelea kijiji ambacho mamia ya watu wengi wao wakiwa wazee na dhaifu walikuwa kwenye mstri mrefu wa kugawiwa chakula.

Watu 14 waliokufa nchini Kenya walikuwa watu wazima, lakini watoto pia wana utapiamlo mkali, mwandishi wa BBC anasema.

Bw Munyes, ambaye ni Waziri wa Kazi katika serikali ya Muungano ya Kenya, alisema idadi ya vifo ingekuwa juu kama Shirika la Msalaba Mwekundu lisingekuwa linagawa chakula cha msaada Turkana.

"Ingekuwa ni janga," alisema.

Bw Munyes alisema vifo hivyo havikusababishwa na upungufu wa chakula bali ni ‘ukosefu wa utaratibu.’

Serikali imeshindwa kusafirisha chakula kwenye vijiji hivyo, alisema.

Mwandishi wa BBC anasema watu wengi Turkana wanahisi wametelekezwa na wametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiangalia kwa makini hali yao mbaya.

Umoja wa Mataifa unasema ukame umesababishwa na ukosefu wa mvua kwa miaka mingi mfululizo.

Umetangaza rasmi kuwa sehemu kadhaa za Somalia zinakabiliwa na njaa.

Karibu raia 1,300 wa Somalia wengi wao wakiwa wanawake na watoto wanaingia nchini Kenya kila siku wakitafuta chakula, Umoja wa Mataifa unasema.