Sudan 'yatishia helikopta ya UN'

Afisa mwandamizi wa umoja wa mataifa amesema, Sudan ilitishia kuidungua helikopta iliyokuwa ikijaribu kuyaondosha majeshi ya kutunza amani ya umoja wa mataifa waliojeruhiwa na mabomu ya ardhini kwenye eneo lenye mgogoro la Abyei.

Mkuu wa majeshi hayo Alain Le Roy alisema umoja huu umetumia saa tatu kujaribu kuishawishi serikali kuruhusu watu hao waondolewe kwa ndege.

Wanajeshi watatu waliojeruhiwa walifariki dunia wakati majadiliano yakiendelea, alisema.

Image caption Majeshi ya kutunza amani ya Umoja wa Mataifa

Majeshi hayo ya kutunza amani yalipelekwa mapema mwezi huu huko Abyei, eneo linalozozaniwa na Sudan na taifa jipya la Sudan Kusini.

Siku chache tu baada ya kufika Ethiopia, msafara wao uligonga mabomu hayo ya ardhini huko Mabok, kusini-mashariki mwa mji wa Abyei.

Mwanajeshi mmoja alikufa papo hapo wakati wengine watatu walifariki dunia baadae, alisema Bw Le Roy, msaidizi katibu mkuu wa majeshi ya umoja wa mataifa.

Alisema, " Hatukuruhusiwa kuondoa helikopta hiyo aina ya Medivac haraka iwezekanavyo."

"Walituzuia kuondoka kwa kututishia kuwa wataidungua helikopta."

Bw Le Roy alisema "hakuna anayeweza kusema" iwapo kuchelewa kuwaondosha wanajeshi hao kwa ndege kulichangia kwa vifo vyao.

Alisema, uchunguzi unafanywa kutokana na tukio hilo.