Arsena na Udinese Ubingwa wa Ulaya

Arsenal imepangwa kukipiga na Udinese katika mechi za kutafuta timu zitakazoingia kwenye makundi ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.

Image caption Arsene Wenger

The Gunners kama wanavyojulikana zaidi kwa mashabiki wao, wataanza kampeni hiyo nyumbani kwao uwanja wa Emirates dhidi ya timu hiyo ya Italia siku ya Jumanne tarehe 16 Agosti, na mchezo wa marudio utafanyika baada ya siku saba zijazo.

Bayern Munich watacheza na FC Zurich, FC Twente ya Uholanzi wataoneshana kazi na Benfica na Lyon watapepetana na Rubin Kazan ya Urusi.

Arsenal wanamatumaini ya kuungana na Manchester United, Chelsea na Manchester City katika mechi za makundi.

The Gunners wanakabiliana na kibarua cha kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Ubingwa wa Ulaya kwa msimu wa 14 kwa sababu msimu uliopita wa ligi ya England walimaliza nafasi ya nne.

Katibu wa klabu ya Arsenal David Miles amesema Gunners wamefurahi kuepuka safari ndefu hadi Urusi kumenyana na Rubin Kazan.

"Itakuwa kibarua kigumu. Lakini hatutawadharau Udinese kabisa. Upangaji ulivyokwenda unatupa nafasi kwa mechi ya kwanza nyumbani na tuna matumaini tutautumia vyema," alisema Miles.

Udinese, walimaliza msimu wa ligi iliyopita ya Italia - Serie A kwa kushika nafasi ya nne. Msimu huu timu hiyo ilimuuza winga wake hatari Alexis Sanchez kwa klabu ya Barcelona, pia kiungo wa kutumainiwa Gokhan Inler kwa klabu ya Napoli.

Meneja mkuu wa Udinese Franco Collavini amesema: "Tunafanya kazi kubwa kukamilisha usajili wa klabu yetu itakapofika tarehe 31 mwezi wa Agosti.

"Tutahakikisha tunafanya kila liwezekanalo kuiandaa timu yetu kwa njia bora zaidi. Tunaiheshimu Arsenal. Ni moja ya vilabu muhimu Ulaya."

Wakati Aersenal walipotolewa katika Ligi ya Ubingwa wa Ulaya mwezi Machi dhidi ya Barcelona, mpachika mabao hodari wa timu hiyo Robin van Persie alioneshwa kadi ya manjano kwa kupiga mpira langoni baada ya mwamuzi Massimo Busacca kupuliza filimbi ya kuashiria ameotea.

Kutolewa huko kwa Van Persie ina maana hatacheza mchezo wa kwanza dhidi ya Udinese, wakati kiungo Samir Nasri pia alifungiwa na Uefa baada ya kutoa maneno makali kwa mwamuzi huyo Busacca.

Mechi ya kwanza ya Arsenal dhdi ya Udinese itakuwa katikati ya mechi yao ya kwanza ya kufungua msimu wa Ligi Kuu ya Soka ya England dhidi ya Newcastle na pia mechi yao na Liverpool katika uwanja wa Emirates, Jumamosi ya terehe 20 mwezi wa Agosti.

Mechi ya pili nchini Italia itakuwa tarehe 23 Agosti, Arsenal ikiwa njiani kwenda uwanja wa Old Trafford kuikabili Manchester United.

Timu 10 zitakazofanikiwa zitaingia katika makundi kukabiliana na timu zilizofuzu moja kwa moja, ambapo makundi yatapangwa mjini Monaco tarehe 25 Agosti.

Timu za kufuzu hatua ya makundi zimepangwa ifuatavyo:

Wisla Krakow v Apoel Nicosia

Maccabi Haifa v Genk

Dinamo Zagreb v Malmo FF

FC Copenhagen v Plzen

BATE v SK Sturm Graz

Odense BK v Villarreal

FC Twente v Benfica

Arsenal v Udinese

Bayern Munich v FC Zurich

Lyon v Rubin Kazan

Mechi za kwanza zitachezwa kati ya tarehe 16/17 na marudio ni tarehe 23/24 Agosti