Itibari ya Marekani inapungua

Vyombo vya habari vya Uchina vimeilaumu vikali Marekani, baada ya itibari ya Marekani kama mkopaji kushushwa kutoka kiwango cha juu kabisa cha A tatu na kampuni moja inayotoa vipimo hivyo ya Standard and Poor's.

Haki miliki ya picha Reuters

Shirika la habari la taifa la Uchina, Xinhua, lilisema siku za Marekani kuweza kukopa tu ili kuziba upungufu wake, zimekwisha.

Na lilitaka Marekani kuhakikisha kuwa pesa ambazo Uchina imeikopesha Marekani ni salama.

Mchambuzi wa maswala ya uchumi mjini Hong Kong - Francis Lun, Meneja Mkurugenzi wa Lyncean Holdings - anasema hayo yaliyotokea Marekani ni hasara kubwa kwa Uchina na Japani:

"Kwa kupunguziwa hadhi ya uwezo wa Marekani kulipa madeni yake, ina maana kiwango cha riba lazima kipande, kwa sababu mikopo ya Marekani sasa ni A-mbili na ushee, siyo A-tatu.

Serikali ya Marekani itabidi kulipa riba zaidi juu ya mkopo wa taifa, na hivo inamaanisha kuwa kiwango cha riba kikipanda, sehemu ya mkopo wenyewe inapungua.

Uchina imeikopesha serikali ya Marekani dola trilioni moja pointi moja.

Japani imeikopesha dola trilioni moja, na ikiwa bei itapungua kwa asili mia moja tu, basi Uchina itapoteza dola bilioni 11; na Japani itapata hasara ya dola bilioni 10 mara moja."