Waasi Libya ‘bado wanaudhibiti mji'

Image caption Mapigano ya Libya

Mji wa Libya wa Bir al-Ghanam, ulio karibu na Tripoli, unaonekana kuwa bado uko katika udhibiti wa waasi baada ya mapigano ya Jumamosi , lich ya serikali kukanusha mara kadhaa.

Waasi walionekana wakisheherekea baada ya kuudhibiti mji huo kilometa 80 (maili 50) kusini mwa Tripoli, katika mashambulizi yaliyolenga kumaliza mgogoro wa miezi kadhaa.

Mwandishi wa AFP alisema walikuwa bado wanaudhibiti mpaka Jumatatu asubuhi.

Saa chache baadaye, serikali ilisema mji huo umedhibitiwa na maisha ‘yamerudi katika hali ya kawaida.’

Mapigano yaliyoanza Jumamosi yalishuhudia mamia ya waasi wakisonga mbele nje ya Milima ya Mafousa upande wa magharibi, chini kuelekea miji ya ukanda wa pwani.

Kufanikiwa kijeshi magharibi mwa nchi ni muhimu kwa waasi kunawapa nafasi ya kuvishinda vikosi vya Kanali Muammar Gaddafi amabvyo vimewazuia waasi kusonga mbele kutoka kwenye ngome yao ya Benghazi iliyoko mashariki.

Mamia ya watu wameuawa na vikwazo vya anga vya Umoja wa Mataifa vimewekwa tangu machafuko ya kisiasa yaanze kupinga utawala wa Kanali Gaddafi mwezi Februari.