Somalia yahitaji vikosi zaidi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Vikosi vya kulinda amani vya AU

Mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia ametoa wito wa kupelekwa vikosi zaidi vya kulinda amani kupelekwa mjini Mogadishu baada ya wapiganaji wa kiislam kuondoka mjini humo.

Augustine Mahiga alisema vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia vinahitaji kuongezewa nguvu kusaidia serikali kuimarisha mamlaka mjini Mogadishu.

Serikali imesema itatoa msamaha kwa wapiganaji wanaojitoa kwenye kundi la al-Shabaab.

Somalia, kwa miaka 20 imekuwa katika migogoro na imekumbwa na njaa.

Al-Shabab wanadhibiti sehemu kubwa ya Kusini na katikati ya Somalia ikiwemo maeneo yaliyokumbwa na baa la njaa.

Mwishoni mwa wiki kundi hili liliwashangaza wachambuzi wengi lilipotangaza kuondoa vikosi vyake mjini Mogadishu.

'Salimisha silaha'

Bw Mahiga ameiambia BBC anaamini kuwa al-Shabab wamerudisha vikosi vyao nyuma.

"Vyote vikosi vya AU na vya serikali vinahitaji kuongezewa nguvu kwa maana ya askari na vifaa kwa haraka kuimarisha mamlaka katika maeneo yaliyoachwa na al-Shabab," aliiambia BBC katika kipindi chake Focus on Africa.

Umoja wa Afrika una vikosi 9,000 nchini Somalia kati ya 20,000 ulioahidi.

Serikali ya Somalia imezungumzia kuondoka kwa al-Shabab siku ya Jumamosi ikisema wapiganaji hao hawataadhibiwa.

"Wekeni chini silaha zenu na mje kujiunga na watu na jamii," msemaji wa serikali Abdirahman Osman alinukuliwa na shirika la habari la AFP akisema.

Shirika la Wakimbizi la UN SIKU YA Jumatatu lilituma misaada kwa waathiriwa wa njaa mjini Mogadishu, msaada wake wa kwanza katika kipindi cha miaka miatano iliyopita.

Takriban watu 100,000 wameingia mjini Mogadishu katika kipindi cha miezi miwili iliyopita kutafuta chakula.

Ukosefu wa usalama umesababisha ugumu kusambaza vifaa hivyo.