Ripoti mpya kulinda wahudumu wa misaada

Wahudumu wa Shirika la Msalaba mwekundu Haki miliki ya picha AFP

Shirika la Msalaba Mwekundu linatoa ripoti mpya hii leo kwa jina huduma ya afya kwenye hatari. Ripoti hiyo imenukuu kulengwa kwa maafisa wa misaada hususan afya na vituo vya afya katika maeneo yanayokumbwa na vita.

Pia inapendekeza kuwepo na haki ya kuwapa matibabu majeruhi wa vita na wanaotoa matibabu kufanya shughuli zao bila kutishiwa maisha.

Ripoti hiyo imesema vita vimeendelea kuyumbisha shughuli za kutoa matibabu ya kuokoa maisha.

Shirika la msalaba mwekundu lilifanya utafiti wake katika nchi 16 zikiwemo Somalia, Afghanistan, Libya na Colombia. Ripoti hiyo iliyochunguza matukio ya miaka miwili imenakili visa mia sita vya kulengwa kwa madaktari, wauguzi, magari ya kusafirishia wagonjwa na vituo vya afya.

Hata hivyo shirika hilo linasema matukio haya ni machache sana ikilinganishwa na hali halisi, kwani kulengwa kwa vituo vya matibabu kumeendelea kuathiri maisha ya mamilioni ya raia duniani.

Hii ni kwa sababu madaktari husitisha huduma zao pamoja na wauguzi, miradi kama ya kutoa chanjo husimama na matibabu hucheleweshwa au kukosekana kabisa.

Ripoti hiyo imeongeza kwamba japo mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu yamefanyika kama ajali visa vingi vimekuwa vya makusudi.

Kulengwa kwa maafisa wa afya ni ukiukaji wa azimio la Geneva dhidi ya haki za wahudumu wa misaada wakati wa kuokoa maisha.

Kutolewa kwa ripoti hii ni mwanzo wa kampeini ya miaka minne ya shirika la msalaba mwekundu kuyataka makundi hasimu katika maeneo ya vita kuelewa kwamba yako na jukumu la kukubalia majeruhi kupokea matibabu na madaktari kupata nafasi ya kuokoa maisha bila kutishiwa maisha.