Nigeria kuchunguza unyanyasaji wa Jeshi

Jeshi la Nigeria limetakiwa kuchunguza tuhuma za unyanyasaji kwa raia uliofanywa na askari wakati wanapambana na wapiganaji wa kundi la Kiislam kaskazini mashariki mwa nchi. Hatua hiyo ya Waziri wa Ulinzi Bello Mohammed imekuja kufuatia mwanamke mmoja kuuawa kwa risasi siku ya Jumatano wakati askari wakipambana na wanapiganaji wa Boko Haram. Makundi ya kihafidhina yamelishutumu Jeshi kwa kufanya mauaji kinyume cha sheria. Mapigano kuzunguka eneo la Maiduguri yamepamba moto katika wiki za karibuni na kusababisha maelfu ya watu kulikimbia eneo hilo. Bw Mohammed alisema Jeshi limekuwa 'likifanya kazi nzuri sana' katika kulinda maisha na mali za Wanaigeria wa Maiduguri na katika jimbo lote la Borno. "Hata hivyo, mayai machache mabovu miongoni mwao wakati mwingine wanapitiliza katika utendaji wao katika hali hizi na kusababisha kutoridhika kwa baadhi ya raia na hivyo kulivuruta Jeshi zima katika mgogoro. " alisema katika taarifa. Amelitaka Jeshi kuchunguza matukio yote yasiyofaa yaliyotokea 'kinyume cha sheria zinazowahusu raia.' Shirika la Kutetea Haki za Binadamu Amnesty International limesema askari katika kikosi cha Pamoja (JTF) waliotumwa Borno wanahusika na vifo 23 na kuchoma moto soko. Ghasia zililipuka siku ya Jumatano baada ya mwanamke mmoja kuuawa kaskazini mwa mji wa Biu ulio jimbo la Borno na kanisa lilichomwa moto. Kwa mujibu wa taarifa za magazeti alikuwa amebeba mtoto mdogo wakati huo. Bw Mohammed ameamuru Jeshi kufanya uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo. Boko Haram - kwa tafsiri isiyo rasmi kama 'Elimu ya Kimagharibi ni Haramu' limekuwa likiendesha mfululizo wa mauaji na kulipua mabomu nchini Nigeria katika harakati zao zao za kujaribu kuipindua serikali na kuunda taifa la kiislam. Katika miezi michache iliyopita wanajeshi wamekuwa kwa wingi katika eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria wakati serikali ikijaribu kulazimisha kumaliza harakati za kundi hilo la kiislam Boko Haram lenye silaha. Mwandishi wa BBC Mjini Lagos Jonah Fisher anaripoti. Lakini vitendo vya Jeshi vimewatenga mbali na wenyeji, alisema. Wakazi wengi wa Maiduguri sasa wanaliogopa jeshi kuliko Boko Haram. Mwezi mmoja uliopita kundi la wazee wa eneo hilo walitaka askari hao kuondoka. Mwezi uliopita Gavana wa jimbo la Borno Kashim Shettima amekiri kuwa jeshi limefanya makosa kupita kiasi Maiduguri.