Mwanasayansi afungwa kwa kumfanya mtu mtumwa

Ramani ya Tanzania
Image caption Ramani ya Tanzania

Mwanasayansi mmoja aliyepatikana na hatia ya kumweka msichana mmoja kama mtumwa nyumbani kwake amehukumiwa kifungo cha miezi sita gerezani.

Mwanasayasi huyo wa masuala ya HIV Rebecca Balira mwenye umri wa miaka 45, amehukumiwa kwa kumweka Methodia Mathias mwenye umri wa miaka 21 kama mtumwa na vile vile kumpiga.

Mahakama ya Southwark ilifahamishwa kuwa, wakati mmoja katika mzozano Bi Balira alipandwa na hasira kiasi cha kuikata Sidiria aliyokuwa amevaa Bi Mathias kwa mkasi na kumjeruhi.

Bi Balira anaeishi Thamesmead eneo la kusini-mashariki mwa London pia aliagizwa amlipe Methodia pauni elfu tatu.

Bi Balira hakupatikana na hatia ya kumuingiza Bi Mathias Uingereza kinyume na sheria na pia amefutiwa mashtaka mengine ya kumdhuru binti huyo.

Wakati wa kesi hiyo Bi. Mathias alisema kuwa Bi Balira alimleta kutoka Tanzania na kumweka kama mtumwa.

Mahakama ilifahamishwa kuwa Bi Mathias alikuwa anaishi na jamaa za Balira nchini Tanzania na waligharamia maombi yake ya VISA (kibali cha kuingia Uingereza) na tikiti yake ya ndege kusafiri hadi Uingereza.

Lakini anadai kuwa alipowasili nyumbani kwa Balira, alilazimishwa kufanya kazi kama mtumwa. Bi Mathias ametoa madai hayo baada ya kuishi na Bi Balira kwa kipindi cha miezi sita.

Mahakama ilifahamishwa kuwa baada ya hapo rafiki yake Mathias aliwasiliana na shirika la Kalayaan linalowasaidia wafanyakazi wa nyumbani kutoka mataifa ya nje waishio hapa Uingereza.

Kate Roberts wa shirika la Kayalaan aliongeza kusema kesi kama hizi huwa zinawapa wasiwasi kuwa, matukio kama haya yanaweza kuongezeka ikiwa ulinzi uliopo sasa katika VISA za wafanyakazi wa nyumbani wageni utaondolewa.