Wapiganaji Libya wadai kuiteka Zawiya

Nchini Libya kuna taarifa za kutatanisha kuhusu nani anadhibiti mji wa kando ya pwani wa Zawiya, kilomita 30 nje ya mji mkuu, Tripoli.

Haki miliki ya picha AP

Wapiganaji waliingia katika mji huo jana, lakini wakuu wa Tripoli wamedai kuwa bado wanaidhibiti Zawiya kikamilifu.

Ikiwa wataiteka Zawiya huo utakuwa ushindi mkubwa kwa wapiganaji.

Mji huo ni jirani na mji mkuu, na uko kwenye barabara inayotoka Tunisia, njia muhimu kwa Kanali Gaddafi.

Ni wazi kuwa wapiganaji wameweza kuingia mjini humo jana, ingawa walipigwa mizinga na risasi.

Ripoti moja kutoka Zawiya kwenyewe, ilisema wapiganaji walikaribishwa na mamia ya wenyeji.

Wapiganaji wanadai kuwa usiku ulipoingia, walikuwa wameshaudhibiti mji.

Wakuu mjini Tripoli wamesema shambulio la wapiganaji lilikuwa dogo tu na kudai kuwa bado wanaudhibiti mji wa Zawiya.