Mabeki watau wa Manchester United waumia

Manchester United imepata pigo la aina yake baada ya mabeki wake watatu wa kutumainiwa Rio Ferdinand, Nemanja Vidic na Rafael da Silva kuumia na hawataweza kucheza kwa muda fulani wakati huu hekaheka za ligi zikiwa zimeanza.

Image caption Rio Ferdinand

Ferdinand hataweza kucheza kwa muda wa wiki sita baada ya kutolewa uwanjani kutokana na matatizo ya msuli wa paja wakati walipoilaza West Brom siku ya Jumapili kwa mabao 2-1.

Vidic, ambaye kama ilivyokuwa kwa Ferdinand naye alitolewa katika mechi hiyo na hatacheza mechi ifuatayo baada ya kuumia goti.

Rafael anaonekana hatacheza kwa muda mrefu zaidi wa wiki 10 baada ya bega lake kuchomoka.

Katika mechi waliyonyakua Ngao ya Hisani kwa kuilaza Manchester City mabao 3-2 wiki iliyopita, Rafael alicheza akiwa mchezaji wa akiba lakini akaumia mazoezini.

Tatizo la kuumia Ferdinand ina maana hataweza kucheza soka hadi mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba na atakosa mechi ya kufuzu kwa England kwa masindano ya Euro 2012 dhidi ya Bulgaria na Wales.

Kwa upande wa klabu atakosa mechi za nyumbani Manchester United itakazocheza dhidi ya Tottenham, Arsenal na Chelsea na mbili za ugenini dhidi ya Bolton na Stoke. Wakati huohuo Rafael pamoja na kukosa mechi hizo pia hataweza kucheza mechi nyingi zaidi zikiwemo dhidi ya Liverpool na Norwich pia mechi dhidi ya watani wao wa jadi Manchester City.

Kuumia kwa walinzi hao kutaleta mabadiliko ya safu ya ulinzi wa timu hiyo ambapo Patrice Evra, aliyekosa mechi ya Jumapili atarejea nafasi yake ya kushoto, huku Fabio atapelekwa ulinzi wa kuume na halafu Phil Jones, Chris Smalling na Jonny Evans watacheza nafasi ya ulinzi wa kati.

Akiwa ameweza kucheza bila ya winga Antonio Valencia na washambuliaji Javier Hernandez na Michael Owen dhidi ya West Brom, Meneja wa United Sir Alex Ferguson amesema: "Tumo katika kipindi kigumu cha kuwa na majeruhi wengi.

Siku ya Ijumaa Ferguson alisema Hernandez, ambaye alipoteza fahamu, ana kama wiki moja kabla hajaweza kurejea mazoezini.

Mlinzi wa zamani wa timu ya Arsenal Lee Dixon anaamini kukosekana kwa Ferdinand na Vidic kutazidi kuongeza changamoto kwa mlinda mlango David de Gea, ambaye alifungwa bao rahisi kipindi cha kwanza dhidi ya West Brom.