Viongozi wa Kiislamu waijadili Somalia

Viongozi na maafisa kutoka nchi 57 wanachama wa jumuia ya nchi za Kiislamu, wamekutana mjini Istanbul kuzungumzia njaa nchini Somalia. Mkutano huo umeitishwa na serikali ya Uturuki.

Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan pamoja na mkewe wanakusudia kuzuru Somalia baadae wiki hii ili kuitanabahisha dunia juu ya hali halisi wanayokabiliana watu wa Somalia.

Kwa serikali ya Uturuki kutumia muda wake mwingi kwa maswala ya Somalia ni ushahidi wa azma ya nchi hiyo ya kutanua ushawishi wake barani Afrika na katika nchi za Kiislamu licha ya kukabiliwa na migogoro kadhaa kwingineko kama vile mzozo katika nchi jirani ya Syria na machafuko katika eneo la wakurdi la kusini Mashariki .

Lakini wananchi wa Uturuki wameitikia vilivyo wito wa kusaidia wanaokabiliwa na maafa nchini Somalia kwa kutoa zaidi ya dola millioni mia moja za kimarekani.

Waziri mkuu Recep Tayyip Erdogan ameahidi kwenda Somalia baadae wiki hii pamoja na waziri wa mambo ya nje na wake zao.

Ziara za viongozi wa serikali ni nadra sana nchini Somalia.

Mkutano huu wa nchi za kiislamu uliitishwa na Uturuki li kuhimiza nchi ziongeze misaada yao na kuonyesha uungaji mkono kwa nchi za kiislamu wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Pia unasadifiana na malengo ya Uturuki barani Afrika ambako imeongeza idadi ya balozi zake katika miaka mitatu iliyopita na pia biashara yake kuongezeka kwa zaidi ya dola billioni saba kila mwaka.