Msaada wa Somalia utafika kwa walengwa

Image caption Bw Andrew Mitchell

Uingereza "haitovumilia" ufisadi unaozuia jitihada za kupambana na njaa Somalia, waziri mwandamizi mmoja alisema.

Andrew Mitchell alisema alizungumzia suala hilo na waziri mkuu wa Somalia alipotembelea nchi hiyo siku ya Jumatano.

Alisema umma wa Waingereza unaochangia fedha katika wiki za hivi karibuni unahakikishiwa msaada unawafikia wale wanaostahili na si kufikishwa kwa wasiokusudiwa.

Serikali hiyo imeahidi dola za kimarekani milioni 25 zaidi kwa ajili ya chakula na dawa kusaidia watu 400,000 ambao wako katika hatari ya kufariki dunia.

Bw Mitchell alikuwa akizungumza baada ya kurejea kutoka mji mkuu wa Somalia ulioathirika na vita- ziara ya kwanza iliyofanywa na waziri kutoka Uingereza kwa kipindi cha miaka 18.

Ameonya kuwa "wanakimbizana na muda" kutatua ukame uliokithiri nchini humo na bila hatua za haraka maelfu ya watoto wanaweza kufa kwa njaa.