Tanzania yapiga marufuku uuzaji wanyama

Twiga
Image caption Twiga

Tanzania imetangaza kuwa inapiga marufuku biashara ya kukamata na kuwasafirisha wanyamapori kwenda nje ya nchi.

Hatua hiyo imetangazwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akijibu hoja bungeni kuhusu madai kwamba wanyama takriban 130 wakiwemo ndege 16 walitoroshwa kinyume cha sheria mwishoni mwa mwaka jana na kusafirishwa kwenda nchi moja ya Mashariki ya Kati.

Katika jibu lake Bw Pinda alisema: “Kwanza tunataka tukubaliane na mawazo ya wabunge kwa ujumla kwamba, inaonekana eneo hili bado utaratibu wake wa usimamizi na hata namna biashara yenyewe inavyofanyika, ni eneo ambalo kwa kweli linahitaji kutazamwa upya.

“Kwa hiyo, kama serikali tumeamua kwamba, tutasimamisha usafirishaji au biashara za wanyama zote na tuangalie tena upya jambo hili na ikitokea kwamba tunakubaliana tuendelee nalo, ni dhahiri na lazima masharti yabadilike.”

Wabunge wa chama tawala pamoja na upinzani wamekuwa wakiishutumu serikali kwa kuifumbia macho kashfa hiyo.

Lakini kwa uamuzi iliofanya, serikali imeonekana kujipunguzia shutuma na kupata kuungwa mkono na wabunge wa kambi zote mbili.

Shutuma

Hata hivyo hitimisho hilo halikufikiwa bila serikali kujeruhiwa vibaya na wabunge. Hoja hizo nzito zilianza kusikika tangu mwanzoni mwa mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara ya maliasili na utalii kwa mwaka 2011/2012.

Haki miliki ya picha Caters
Image caption Wanyama katika mbuga ya Tanzania

Mbunge Christopher Ole-Sendeka wa jimbo la Simanjiro kupitia chama tawala cha CCM alisema tukio hilo limeidhalilisha serikali na vyombo vyake vya dola vyenye majukumu ya kusimamia usalama wa nchi.

“Kinachotia fedheha kuliko yote ni kwamba, waliofanya kazi hiyo walipewa zawadi nyingine ya kupandishwa vyeo. Nataka niseme wazi kuwa mkurugenzi wa wanyamapori wa sasa, ndugu Mbangwa, hawezi kukwepa lawama ya kutoroshwa wanyama hao,” alisema Ole Sendeka aliyeonekana kuungwa mkono na wenzake.

Hatua za serikali

Habari za kutoroshwa wanyama zilianza kusikika tangu mwanzoni mwa mwaka huu, lakini mjadala wa bajeti ya Wizara ya maliasili na utalii ndiyo imeibua maswali mazito dhidi ya serikali ambayo imelazimika kutoa majibu na kuchukua hatua.

Waziri wa maliasili na utalii Ezekiel Maige aliposimama kujibu hoja zilizotolewa na wabunge wa pande zote mbili alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema serikali imekuwa ikilifanyia uchunguzi kwa muda wa miezi kadhaa.

Vile vile waziri huyo alitangaza kuwasimamisha kazi maafisa waandamizi wa Idara ya wanyamapori, akiwemo mkurugenzi mkuu Obeid Mbangwa, ili kuwezesha uchunguzi ufanyike kubaini swala hilo lilifanyika katika mazingira ya gani.

Tanzania inategemea utalii kwa asilimia takriban 17 ya mapato yake, ambapo kwa mwaka huu utalii unatarajiwa kuvuna dola bilioni 1.7. Wanyama ni sehemu muhimu ya vivutio vya Tanzania.