Kinshasa inawasha mishumaa

Makundi ya wanaharakati katika Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, yametoa wito kwa wakaazi wa mji mkuu, Kinshasa, kuwasha mishumaa leo usiku, kulalamika juu ya kukatwa kwa umeme.

Ingawa Congo ina miporomoko ya maji inayoweza kuzalisha umeme mwingi, hata hivo mitambo iliyochakaa na kina cha maji kupungua kwenye mabwawa makuu, kumepunguza umeme na hivo kuathiri biashara, hospitali na shughuli nyengine.

Kila mmoja kati ya wakaazi milioni 10 wa Kinshasa wameombwa wawashe mishumaa wakati mmoja, kwenye barabara, nyumba, maduka na roshani.

Wanaharakati wanataraji mishumaa italeta mwangaza katika mji ambao mara nyingi uko gizani.

Wasiokuwa na mishumaa wameshauriwa kugonga sufuria.