Villas-Boas ampongeza Mata wa Valencia

Meneja wa Chelsea Andre Villas-Boas amempongeza kiungo wa Valencia Juan Mata, huku kukiwa na taarifa yu-karibu kusajili na klabu ya Chelsea.

Image caption Juan Mata

Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Hispania zimesema mchezaji huyo wa Valencia mwenye umri wa miaka 23, anajiandaa kujiunga Stamford Bridge kwa kitita cha paundi milioni 23.5.

Baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya West Brom siku ya Jumamosi, Villas-Boas ana uhakika wa kumsajili Mata.

Amesema: "Ni mchezaji anayefunga mabao na kusaidia kutengeneza mabao kwa wengine na anaweza kucheza katika kikosi chochote duniani."

Villas-Boas ameongeza: "Si mchezaji wetu kwa sasa lakini anavutia.......ni mchezaji mzuri sana."

Mata amekuwa katika kikosi cha Valencia tangu mwaka 2007 na ameisaidia timu ya taifa ya Hispania chini ya umri wa miaka 21 kuweza kushinda Ubingwa wa Ulaya mwaka huo.

Villas-Boas awali alizungumzia umuhimu wa kusajili wachezaji wa kiungo na klabu hiyo pia bado inamuwinda kiungo wa Tottenham Luka Modric.