Ferguson amsifu mshambuliaji Welbeck

Meneja wa Manchester United Sir Alex Ferguson amesifu Danny Welbeck pamoja na kikosi chake cha vijana baada ya ushindi mnono wa mabao 3-0 dhidi ya Tottenham.

Image caption Danny Welbeck

Mshambuliaji huyo, aliyefunga bao la kwanza katika dakika ya 61 kwenye uwanja wa Old Trafford siku ya Jumatatu, alikuwa katika kikosi cha kwanza kilichoanza mechi hiyo wengi wakiwa na umri wa wastani usiozidi miaka 23.

"Kundi hili ni uwezo wa ajabu, kwa kweli wananifanya nikubali kuwachezesha," alisema Ferguson.

"Danny bado ana umri wa miaka 20 tu na anaweza kucheza vizuri sana miaka mingi ijayo."

Welbeck alivutia zaidi katika kipindi cha pili baada ya kipindi kigumu cha kwanza, wakati alipopata shida ya kumiliki mpira.

"Nahisi kipindi cha kwanza, Danny hakucheza kama mshambuliaji wa kati," aliongeza Ferguson.

Welbeck amepata mafanikio akitokea timu za vijana wa Manchester United na alifanikiwa kucheza timu ya wakubwa mwaka 2008 katika mechi dhidi ya Middlesbrough.

Alicheza kwa mkopo katika klabu ya Preston mwanzoni mwa mwaka 2010 kabla ya kujiunga na Sunderland kwa msimu mzima wa 2010-2011.