Sudan yatangaza kusitisha mapigano

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kordofan Kusini

Rais wa Sudan ametangaza kusitisha mapigano kwa wiki mbili kwenye jimbo la Kordofan kusini kufuatia mapigano yaliyoanza tangu Juni na kusababisha takriban watu 70,000 kuhama makazi yao.

"Natangaza kusitisha mapigano pande zote mbili kwa kipindi cha wiki mbili," Shirika la habari la AFP limemnukuu Omar al-Bashir akizungumza kupitia radio ya taifa.

Mgogoro huo ulianza baada ya serikali kujaribu kuwanyang'anya silaha wapiganaji wa kabila la Wanubi baada ya uchaguzi katika jimbo linalopakana na nchi mpya ya Sudan Kusini.

Khartoum imekana madai ya mauaji ya kimbari dhidi ya wanaounga mkono Wanubi wa kusini.

Mwandishi wa BBC James Copnall kwenye mji mkuu, Khartoum, alisema mapigano yamepungua Kordofan Kusini mwezi huu kutokana na mwezi mtukufu wa Ramadhan.