AU kujadili kuutambua uongozi wa waasi

Waasi Libya Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Waasi nchini Libya

Viongozi wa Muungano wa Afrika wanakutana mjini Addis Ababa Ethiopia, kujadili mzozo nchini Libya.

Katika mkutano huo viongozi hao watazingatia iwapo watabue utawala wa serikali ya mpito inayoongozwa na waasi.

Lakini kama anavyotathmini Mhariri wa BBC wa Kitengo cha Afrika, Solomon Mugera, ''huenda uamuzi wao usiwe na uzito wowote''.

Kuna mgawanyiko mkubwa kati yao, kwanza kuhusu uhalali wa hatua ya kivita ya NATO na pia wamegawanya kuhusu nini itakuwa hatima ya Kanali Muammar Gaddafi.

Kwa miaka mingi, Gaddafi amekuwa akitumia mamilioni ya dola kujipendekeza kwa viongozi wa Afrika na wakati mwingine kuunga mkono harakati za uasi katika nchi mbalimbali za Afrika.

Marafiki wa Libya watoroka

Huku utawala wake ukiendelea kuporomoka, waliokuwa marafiki zake miongoni mwa viongozi wa Afrika, nao pia wanamtoroka.

Baadhi ya nchi kama vile Senegal, Nigeria, Ethiopia, Chad na Botswana zimetangaza wazi kwamba zinawatambua waasi nchini Libya. Huenda hata matokeo ya mkutano wa leo wa AU yasiwe na ushawishi wowote kuhusu hali ilivyo kwa sasa au hata mnamo siku zijazo nchini Libya.

Umoja wa Afrika umekuwa ukilalamika hadharani kwamba mataifa tajiri yamekuwa yakipuuza mchango wowote wa AU kuhusu mzozo wa Libya.

Isitoshe, uhusiano umedorora kati ya Muungano wa Afrika na waasi wanaotawala sehemu muhimu nchini Libya.

Kwa kuwa waasi wanapata msaada wa kifedha na kivita kutoka kwa NATO na nchi za Magharibi, hawaoni manufaa yoyote ya Muungano wa Afrika - hasa ikizingatiwa kwamba Muungano huo umekuwa ukifadhiliwa kwa kiasi kikubwa na Kanali Gaddafi.

Pesa Gaddafi alizowekeza nje

Halitakuwa tukio la ajabu iwapo waasi wataanza kudai mamilioni ya fedha ambazo Gaddafi aliwekeza binafsi au kupitia shirika la uwekezaji la Libya katika biashara ya mafuta au hoteli za kifahari.

Tayari ombi la Marekani la kuondoa tanji dhidi ya rasilimali za Libya limekubaliwa.

Afrika Kusini ambayo ilikuwa ikipinga ombi hilo imesalimu amri baada ya kuwepo na hakikisho kwamba pesa hizo zitatolewa kwa maslahi ya kibinadamu na sio moja kwa moja kwa harakati za waasi.

Ukizingatia hatua hiyo, ni dhahiri kwamba Muungano wa Afrika utalazimika kutambua utawala wa waasi.