Mkutano wa AU wafanyika kuhusu njaa

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika, Jean Ping

Umoja wa Afrika unafanya mkutano wake uliocheleweshwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kuahidi pesa za kupambana na njaa iliyoikumba Pembe ya Afrika.

Umoja huo tayari umeahidi $500m (£300 milioni), lakini Umoja wa Mataifa unasema takriban kiasi kingine $2bilioni kinahitajika kusaidia tatizo hilo.

Takriban watu 12 million nchini Somalia na nchi jirani zinahitaji msaada wa dharura, Umoja wa Mataifa umesema.

Shutuma za kuchelewa kusaidia

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Afrika Jean Ping ametoa wito kwa waafrika ‘kuamka na kupambana na njaa kwa kutoa pesa na mali ili kusaidia na kuokoa ndugu na dada zetu wa Pembe ya Afrika ".

Marekani, Uingereza, China, Japan, Brazil na Uturuki zote zimeahidi kutoa fedha kwa eneo hilo kama ilivyofanya Jumuiya ya nchi za Kiislam OIC inayoundwa na nchi za Kiislam lakini michango hiyo imepungua kiasi kilichoombwa.

Waandishi wanasema serikali kadhaa za Afrika zimeshutumiwa kwa kukosa kuchukua hatua mapema, na Shirika La misaada la Oxfam linasema ni nchi chache tu za Afrika ndio zimechangia pesa mpaka sasa.

Uhaba wa chakula unatajwa kuwa tatizo sugu linaloathirir bara zima tangu njaa ya mwaka 1991-1992.