Waasi waelekea mji wa Gaddafi

Gaddafi Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Picha ya Gaddafi

Waasi wa Libya wanasonga mbele kuelekea katika mji wa Sirte alipozaliwa Kanali Gaddafi, baada ya kuuteka karibu mji wote wa Tripoli.

Wamekuwa wakipambana vikali na takriban wapiganaji 1,000 wanaomtii Gaddafi, katika barabara inayoelekea katika mji huo wa mashariki, ambao bado unadhibitiwa na wanaomtii Gaddafi.

Janga

Kuna taarifa za mappigano mapya mjini Tripoli, ambao umekuwa kimya usiku kucha.

Kiongozi wa serikali ya waasi Mahmoud Jibril ametoa wito wa kutolewa misaada ya haraka kukabiliana na janga la kibinaadam.

Mahitaji muhimu na umeme vimeanza kupungua, hali ambayo serikali inayosubiri kuingia madarakani inasema huenda ikasababisha kutetereka kwa hali ya utengemano.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Waasi wakielekea Sirte

Umoja wa Mataifa unatarajiwa kupiga kura wiki hii, kupitisha muswada wa kuruhusu dola bilioni 1.5 za amana ambazo zilikuwa zimepigwa tanji chini ya vikwazo vilivyowekwa.

Takriban dola milioni 500 zimetolewa, lakini Afrika Kusini imekwaza juhudi za Marekani kutoa fedha zaidi, ikisema inataka kupata maelekezo kutoka Umoja wa Afrika, ambayo haijautambua utawala wa waasi.

Wapiganaji wa waasi wanaoelekea Sirte wanasemekana kuzuiwa katika mji wa Bin Jawad kutokana na wanaomtii Gaddafi kusimama imara.

"Wapiganaji wa Gaddafi bado wanapigana, tunashangaa," amesema kamanda wa waasi Fawzi Bukatiff, akikaririwa na shirika la habari la AFP.

"Tulidhani watajisalimisha baada ya Tripoli kuchukuliwa."

Kimya

Jumba la Kanali Gaddafi liitwalo Bab al-Aziziya liliingiliwa siku ya Jumanne, ingawa kulikuwa na mapigano ndani ya jumba hilo siku ya Jumatano.

Mji mkuu Tripoli ulikuwa kimya siku ya Alhamisi asubuhi lakini mapigano yalizuka tena mchana. Kuna taarifa za mapigano katika wilaya ya Abu Salim na karibu na hoteli ya Corinthia, takriban kilomita 1.5 kutoka eneo la wazi lililojulikana kama Green square, ambapo waandishi wengi wa habari wa kimataifa wameweka maskani.