Vituo vya Polisi na Benki vyashambuliwa Nigeria

Image caption Shambulio la Boko haram Nigeria

Takriban watu 12 wameuawa katika shambulio kwenye benki mbili na vituo viwili vya polisi katia mji wa Gombi jimbo la Adamawa kaskazini mwa Nigeria.

Maafisa katika eneo hilo wanasema huenda kundi la Kiislam la Boko Haram limehusika na mashambulio hayo siku ya Alhamisi.

Polisi, wafanyakazi wa baenki na wateja wameuawa, huku waliofanya shambulio hilo wakikimbia na silaha na fedha, ripoti zinasema.

Boko Haram, liliundwa mwaka 2002, linapigania kuwepo utawala wa Kiislam nchini Nigeria.

Mkazi wa Gombi, Husseini Abdurrazak, alisema aliwaona watu wenye silaha wakivamia kituo cha polisi na kutoroka na silaha kabla ya kuiba kwenye benki, shirika la Habari la AFP limeripoti.

"Walikuwa wakiimba 'Allahu Akbar' na tunahisi huenda wanaweza kuwa wanachama wa Boko Haram au ni wezi tu wenye silaha waliojifichia kwenye kundi hilo," alisema.

Majadiliano

Mwandishi wa BBC Abdullahi Kaura Abubakar mjini Kaduna anasema mamlaka katika eneo hilo wanaamini huenda watu hao wenye silaha ni kutoka Boko Haram.

Kundi hilo limekubuhu kwa mashambulizi ya vituo vya polisi na mabenki kaskazini mwa Nigeria kuendesha harakati zake, mwandishi wetu anasema.

Miaka miwili iliyopita, vikosi vya usalama vya Nigeria kikatili vilizima kuinuka kwa kundi hilo, vikiharibu makazi yake mjini Maiduguri, makao makuu ya jimbo la Borno na kisha kumshika na kumuua kiongozi wake Mohammed Yusuf.

Badala ya kutoweka, kundi hilo limeibuka tena mwezi Septemba mwaka jana na kuapa kulipiza kisasi kifo cha kiongozi wake.

Mwezi Juni, Boko Haram lilisema limefanya mashambulizi katika makao makuu ya polisi mjini Abuja na kuua watu sita.

Katika kujibu, vikosi vya usalama vimeanzisha harakati nyingine ya kulivunja kundi hilo wakati Rais Jonathan Goodluck ameteua kamati kufanya uchunguzi wa wazi na viongozi wake.