Tripoli inahitaji msaada

Uingereza inasema itapeleka chakula na madawa Libya, ambayo yanahitajika sana wakati mapigano yanaendelea katika hatua ya mwisho ya kumuondoa Kanali Gaddafi ambaye amejificha.

Haki miliki ya picha AP

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, anasema upungufu wa vitu muhimu katika mji mkuu, Tripoli, unahatarisha maisha.

Sehemu kubwa ya Tripoli haina maji, mahospitali hayana dawa za kutosha, na chakula na mafuta ni shida kupatikana.

Juma zima hili maji ya bomba katika mji mkuu yamekuwa yakikauka taratibu.

Karibu Tripoli nzima sasa haina maji na sehemu nyingi hakuna umeme.

Baadhi ya maduka yanafunguliwa lakini hayakupata shehena siku kadha.

Petroli na diesel inapungua.

Barabarani kuna mirunda ya taka.

Baadhi ya hospitali zinafanya kazi sawasawa lakini moja, kwenye mtaa wa Abu Salim, ambako mapigano bado yanaendelea, imehamwa na madaktari na wauguzi waliokuwa na hofu.

Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu limekuta maiti zikiooza za wagonjwa 200 waliokufa.

Serikali inayochukua madaraka ya Baraza la Taifa la Mpito, inadai kuwa sasa inadhibiti asili mia 95 ya mji mkuu, lakini mapigano yanayoendelea na khofu iliyokuwako, inaumiza sana mji.