Mo Farah akosa dhahabu mita 10, 000

Mo Farah wa Uingereza ameshindwa kunyakua medali ya dhahabu katika mbio za mita 10,000 za Ubingwa Dunia baada ya kupitwa sekunde za mwisho kabla ya mfundo na Muethiopia Ibrahim Jeilan.

Image caption Mo Farah

Farah, ambaye ni binadamu mwenye kasi zaidi duniani mwaka huu katika mbio hizo za mita 10,000 zenye mizunguko 25, alikuwa amelenga kuwa Muingereza wa kwanza kushinda medali ya dhahabu katika mbio hizo ndefu.

Katika mbio hizo alionekana kujiamini sana akiongoza mbio hizo hadi iliposalia chini ya mizunguko miwili.

Lakini ameiambia BBC: "Inauma. Kila mara unahitaji kushinda dhahabu. Hatimaye nimeambulia patupu."

Farah alikuwa akiongoza mbio hizo sehemu kubwa na alionekana hana wasiwasi huku akiongeza kasi zikiwa zimesalia mita kama 600.

Lakini Jeilan polepole alianza kupumua mgongoni mwa Farah walipokuwa wakiingia hatua ya mwisho na akampita Farah huku wakiukodolea macho mstari wa kumalizia.

Mwenzake Jeilan kutoka Ethiopia Imane Merga alishika nafasi ya tatu na kunyakua medali ya shaba, lakini Kenenisa Bekele, mshindi wa mbio za mita 10,000 kwa miaka minne iliyopita hakumaliza mbio hizo ikiwa imesalia mizunguko 10 kutokana na kuumia.

Bingwa huyo mara tatu wa Olympic Bekele, hajashiriki mbio zozote tangu mwezi wa Januari mwaka 2010 kutokana na kuumia na hakuonekana kama angetoa changamoto ya kuwania medali.