Stoke yakwama kumsajili Lukaku wa Chelsea

Stoke imekwama katika mipango yake ya kutaka kumsajili kwa mkopo mshambuliaji mpya wa Chelsea Romelu Lukaku kwa sababu ya kanuni za Ligi Kuu ya England.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Romelu Lukaku

Romelu Lukaku, aliwasili Stamford Bridge akitokea klabu ya Anderlecht mapema mwezi wa Agosti na alicheza mechi yake ya kwanza na Chelsea siku ya Jumamosi.

Lakini kanuni ya Premier League namba M 7.1 inasema: "Usajili wa muda hautawezekana wakati wa dirisha la usajili ambapo mchezaji amekuwa ndio kwanza amekamilisha usajili na klabu nyingine."

Wakati huo huo Stoke wamo mbioni kumsajili Wilson Palacios kutoka Tottenham kwa kitita cha paundi milioni 6 na kiungo huyo anajiandaa kufanyiwa uchunguzi wa afya yake.

Stoke katika siku za karibuni pia imehusishwa kutaka kumchukua mshambuliaji wa Spurs Peter Crouch.

Na vyombo vya habari vya Denmark vimesema mshambuliaji wa Arsenal Nicklas Bendtner huenda yupo njiani kujiunga na Stoke.

Chelsea ilimsajili Lukaku kwa kitita cha paundi milioni 20 tarehe 6 mwezi wa Agosti. Ni mchezaji mashuhuri nchini Ubelgiji baada ya kuwa mfungaji bora katika ligi ya nchi hiyo msimu wa 2009-2010 alipokuwa na umri wa miaka 16.

Alifunga mabao 16 katika mechi 37 za ligi msimu uliopita na akafunga bao lake la kwanza katika mechi ya kimataifa Ubelgiji ilipoilaza Urusi mabao 2-0 mwezi wa Novemba.