Malema kuadhibiwa na ANC

Kiongozi wa vijana wa chama tawala cha Afrika Kusini cha African National Congress hii anafikishwa mbele ya kamati ya nidhamu ya chama hicho kwa mashtaka ya utovu wa nidhamu na kusababisha mgawanyiko wa uongozi katika chama cha ANC.

Image caption Julius Malema

Julius Malema, mwenye umri wa 30, pia anakabiliwa na mashtaka ya kuiletea ANC jina baya kwa matamshi yake ya kutaka wapinzani nchini Botswana kuungana dhidi ya utawala wa serikali ya nchi hiyo kwa maelezo kuwa ni ya kibaraka.

Mwanzoni Bwana Malema alikuwa mshirika wamuhimu wa Rais Jacob Zuma, lakini sasa ameonekana kumkosoa Rais huyo na kutotaka apande kipindi cha pili cha uongozi.

Bwana Malema, siku za karibuni amekuwa akikabiliwa na tuhuma mbalimbali ndani ya chama cha ANC, zikiwemo za udanganyifu na rushwa. Malema amesema yuko tayari kukubaliana na maamuzi ya kamati ya nidhamu.

"Sisi tutawajibika kutokana na matendo yetu na tuko tayari kwa lolote daima msimamo wetu ni Kuwa ANC ni maisha yetu ya baadaye, na kama ni kufukuzwa hayo yatakuwa maamuzi ya chama," alisema.

Bwana Malema ambaye anakabiliwa na tuhuma mbalimbali pamoja na wajumbe watano kutoka umoja wa vijana wa ANC, wanaweza kufukuza kutoka chama hicho.

Ameshutumiwa na kamati ya nidhamu kwa kujaribu kumkosoa Bwana Zuma mwaka jana.

Kiongozi huyo wa umoja wa vijana ametoa wito wa kutaka sekta ya madini na ardhi kuwanufaisha jamii maskini za wazalendo.

Mwandishi wa BBC Karen Allen ameeleza kwamba Bwana Malema ni "shujaa wa kisiasa", ambapo umoja wa vijana huletea ANC hukipa chama hicho kura 350,000 na una ushawishi juu ya viongozi waandamizi wa ANC wanaotafuta vyeo.

Kesi yake ya kinidhamu ni muhimu kwa ajili ya siasa ya uongozi mwaka kesho, wakati Bwana Zuma anajaribu kupata muhula wa pili wa uongozi.

Mei 2010, Malema alitakiwa kuomba radhi hadharani kufuatia safari ya utata nchini Zimbabwe ambako alitangaza kwamba ANC inamuunga mkono Rais Robert Mugabe wakati huo Bwana Zuma alikuwa mpatanishi kati ya serikali ya Bwana Mugabe na wapinzani wake katika mgogoro wa kisiasa uliokuwa umeikumba nchi hiyo.