Coates akamilisha usajili na Liverpool

Liverpool imekamilisha kumsajili mlinzi wa kimataifa wa Uruguay Sebastian Coates akitokea klabu ya Nacional.

Image caption Sebastian Coates

Coates mwenye umri wa miaka 20 alikuwa mchezaji nyota wa Uruguay katika mashindano ya Copa America mwezi wa Julai na amesaini mkataba wa muda mrefu katika Anfield.

Mlinzi huyo wa kati mwenye urefu wa futi 6 na inchi 6, alifaulu vipimo vya afya yake na amekwishapata kibali cha kufanyia kazi na anakuwa mchezaji wa sita kusajiliwa na Liverpool msimu huu.

Anaungana na mchezaji mwenzake wa Uruguay Luis Suarez, ambaye aliandika katika mtandao wa tweeter: "Ningependa kumkaribisha Anfield, Coates mwenzangu katika timu ya taifa ya Uruguay, rafiki na mchezaji bora," .

Meneja wa Liverpool Kenny Dalglish alikuwa na shauku ya kuimarisha ngome yake baada ya mlinzi Sotirios Kyrgiakos kujiunga na klabu ya Wolfsburg akiwa mchezaji huru.

Manchester City nayo ilihusishwa sana kutaka kumchukua Coates, lakini sasa amejiunga na kikosi cha Liverpool ambacho hivi karibuni kiliwapata wachezaji wa kiungo Jordan Henderson, Charlie Adam na Stewart Downing, mlinda mlango Doni na mlinzi Jose Enrique.