Kaka wa Rais Togo wafikishwa mahakamani

Image caption Faure Gnassingbe, Rais wa Togo

Kaka wa kambo wawili wa Rais wa Togo wamefikishwa mahakamani, wakituhumiwa kufanya njama ya kupindua serikali mwaka 2009.

Aliyekuwa waziri wa ulinzi Kpatcha Gnassingbe alikamatwa alipokuwa akitafuta hifadhi kwenye ubalozi wa Marekani baada ya madai ya jaribio hilo la mapinduzi.

Anatuhumiwa kwa kuwa kinara wa kupanga njama ya mapinduzi hayo, pamoja na kaka yake Essolizam.

Faure Gnassingbe alichukua madaraka mwaka 2005 kufuatia kifo cha baba yake, aliyeiongoza Togo kwa miaka 38.

Awali Rais Gnassingbe aliwekwa kuwa kiongozi na chama tawala pamoja na jeshi.

Baada ya jumuiya za kimataifa kulaani kitendo hicho, uchaguzi ukafanyika, ambapo alishinda, licha ya kuwepo malalamiko ya kufanya hila kutoka vyama vya upinzani na waangalizi wa uchaguzi.

Takriban watu wengine 30, akiwemo aliyekuwa mkuu wa majeshi, Assani Tidjani, nao wanatuhumiwa kushiriki katika jaribio hilo la mapinduzi, ambapo watu wawili wanasadikiwa kufariki dunia.

Kesi hiyo inasikilizwa katika mahakama kuu kwenye mji mkuu, Lome.