Watoto wa Gaddafi wahitilafiana

Mwana wa kiume wa Kanali Muammar Gaddafi ambaye ni maarufu sana ameapa kuwa hivi karibuni watapata ushindi licha ya wafuasi wa Gaddafi kupewa makataa ya kujisalimisha na Baraza la Mpito la Libya.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Saif al-Islam Gaddafi

Saif al-Islam Gaddafi amesema alikuwa anazungumza akiwa viungani mwa mji mkuu wa Tripoli na kwamba babake alikuwa salama.

" mapambano bado yanaendelea na ushindi unakaribia", alitangaza kupitia ujumbe wa Radio.

Dakika chache kabla ya tangazo hilo la Saif al-Islam , nduguye mdogo, Saadi alitangaza kuwa ana ruhusa ya babake ya kujadiliana na Baraza la Mpito ili kumaliza vita nchini Libya.

Lakini viongozi wa Baraza hilo la Mpito wametangza kuwa hawana haja na majadiliano yeyote .

Awali Barazi hilo lilikuwa limewapa wafuasi wa Kanali Gaddafi hadi jumamosi kujisalimisha au sivyo washambuliwe vikali.

Makamanda wa waasi wametangazi kuwa kwa wakati huu wanauzunguka mji wa Sirte alikozaliwa Kanali Gaddafi na pia kujitayarisha kushambulia maeneo mengine machache ambayo bado yanadhibitiwa na wafuasi wa Gaddafi.

Lakini katika ujumbe wake uliotangazwa kupitia Radio moja , Saif al-Islam amewaonya waasi wasithubutu kufanya amshambulizi hayo akijigamba kuwa kuna wapiganaji wapatao 20,000 ambao wako tayari kulinda mji huyo wa Sirte.

Wana hao wa Gaddafi siku zote wana mitazamo tofauti, Saif al-Islaam alikuwa maarufu sana na alikuwa anapigiwa upato wa kuchukua uongozi kutoka kwa babake.

Lakini Saadi ambaye amesomea ulaya anasisitiza kuwa amepewa ruhusa na babake kujadiliana na waasi kumaliza umwakikaji wa damu nchini Libya.